December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia akuna wengi sakata la Ngorongoroo

Wasema kitendo cha kutuma wasaidizi wake kwenda kuwasikiliza wananchi
hao na kutoa uamuzi wenye afya ni kielelezo cha ukomavu kwenye uongozi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa usikivu wake ambao umewezesha kusikiliza ushauri wa Watanzania na kutoa maamuzi mbalimbali ikiwemo kurejesha huduma za jamii kwa wananchi wa Kata 11 za Ngorongoro.

Rais Samia ameingilia kati sakata hilo mwishoni mwa wiki ikiwa ni siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kumuomba Rais Samia kama mfariji mkuu kuingilia kati suala la Ngorongoro ili sakata hilo liweze kupatiwa ufumbuzi kupitia meza ya mazungumzo.

Ijumaa wiki iliyopita, Rais Samia alimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, kwenda kuzungumza na wananchi wa kata 11, katika eneo la Oloirobi lililopo Kata ya Ngorongoro, ambapo aliwafikishia ujumbe wa Rais Samia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu uamuzi huo wa Rais Samia, baadhi ya wananchi walisema Rais ameonesha sifa zote za kuwa kiongozi kwa kusikilia ushauri wa Watanzania na kuufanyia kazi kuhusu yanayojiri Ngorongoro.

“Rais Samia angeweza kunyamaza kimya na tusingeweza kumfanya chochote, lakini kwa usikivu wake ameweza kusikiliza Watanzania na ameweza kutuma wasaidizi wake wakiongozwa na Lukuvi, kwenda Ngorongoro kufikisha ujumbe wake,” alisema Nassoro Abbas mkazi wa Dar es Salaam.

Alisema siku zote Rais halazimishwi kufanyia kazi ushauri anaopewa ikiwa anaona jambo linalofanyika lina maslahi mapana kwa kwa nchi.

“Kwa kweli nchi yetu inahitaji kuwa na viongozi wa aina hyo,” alisema Abbas,

Naye Aloyce Paul alisema usikivu aliouonesha Rais na kuamua kupanga siku maalum kwenda kusikiliza wananchi hao ni kielelezo kwamba anajali na anathamini wananchi anaowaongoza.

Paul alitolea mfano wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano lilipotokea tetemeko la ardhi mkoani, pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii kutoa ushauri kwa Rais iliyekuwepo madarakani ili waathirika waweze kusaidiwa, lakini hakuna kilichofanyika.

“Tunakumbuka majibu yaliyotolewa wakati huo sihitaji kuyarudia kwa sababu hayakuwa na afya kwa wananchi wa Kagera na hawakusaidiwa,” alisema na kuongeza;

“Kwa hiyo tunapokuwa na viongozi wasikivu kama Rais Samia basi anastahili kupewa maua yake.

Kwa upande wake, Damian Swai, alisema Uamuzi wa Rais Samia utaendelea kufanya nchi kuwa ya mfano na kielelezo cha falsafa yake ya 4R.

Lukuvi aliambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji.

Kwenye mkutano wake na wananchi hao, Lukuvi alisema wametumwa na Rais Samia kuzungumza nao na kutoa maagizo hayo ambayo ameelekeza mamlaka zote kuanzia mkuu wa mkoa hadi wilaya kuhakikisha yanatekelezwa.

Aidha, Lukuvi alisema Rais Samia amepanga kukutana na wawakilishi wa wananchi hao na kuwa utaratibu wa kukutana nao utaandaliwa ili wakawasilishe kero zao mbele yake.

“Mkurugenzi wa Ngorongoro hawa wananchi wanapata huduma kwenye mamlaka hii lakini ziko baadhi ya huduma hazitolewi vizuri… baadhi ya shule vyoo vyake vimeharibika lakini ninyi hamshughulikii, kuna baadhi ya shule maji hayatoki, kuna shule zimeharibika lakini hamtengenezi,” alisema Lukuvi.

Alisema kuna viongozi ambao wanapata tabu kupita kwenye mageti, wakiwamo wenye magari binafsi ambao huzuiwa baada ya saa 10.30 jioni.

Kutokana na hilo, ametoa maelekezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro kuhakikisha usumbufu huo unaondolewa.

“Huduma za wanafunzi zitolewe kikamilifu, huduma hospitalini lazima zitolewe kikamilifu. Nataka Makonda uhakikishe kule kote ambako huduma zimesitishwa zirejeshwe ili wananchi hawa wasipate shida kupata huduma za kijamii,” alisema.

“Tunazo habari kuna baadhi ya wanafunzi wanajisaidia vichakani, kule shule ya sekondari ya wasichana kuna mashine imeharibika wanafunzi wanakwenda kilomita kadhaa kufuata maji kwenye kisima, nakupa siku saba ile mashine itengenezwe,” alieagiza.

Pia alitoa mwezi mmoja kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha hakuna vyoo kwenye shule yoyote ambavyo vimejaa.

Lukuvi aliongeza kuwa Rais Samia amesikiliza na kusoma mabango yote waliyonayo wananchi hao na kuwa, alipata salamu kutoka kwa viongozi wao na kuwa jitihada zingine alizofanya ni kumtuma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Arusha kuzungumza na wawakilishi wao.

Alisema Rais alisema anahakikishe jamii ya Ngorongoro, kwamba pamoja na kwamba mahakama imetoa uamuzi (Agosti 22) wa kuzuia GN, yeye kama msimamizi wa Katiba na utawala bora, wakati uamuzi unatolewa alishawatuma na kuwa uamuzi huo umeimarisha nia ya Rais.