December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Samia akagua ujenzi jengo la abiria uwanja wa ndege Mpanda

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amefika Mkoa wa Katavi na kuanza kukagua ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege Mpanda ambao unagharimu fedha zaidi ya Bilioni 1.4

Ukaguzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa ziara yake ya kikazi mkoani humo ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekamilika na isiyokamilika ikiwa pamoja na kuhitimisha kilele cha wiki ya wazazi kitaifa ya Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA) Mussa Mbura akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo leo,Julai 12, 2024 katika uwanja wa ndege Mpanda ametoa historia fupi ya uwanja huo kuwa ulianzishwa mwaka 1954 na kuwa kitovu cha kuchochea maendeleo ya uchumi mkoani humo.

Mbura amesema kuwa tangu mwaka 1954 serikali imekuwa ikifanya maboresho ya mara kwa mara ya kiwanja cha ndege Mpanda kulingana na mahitahi ya kipindi husika ili kuendana mabadiliko ya kisasa.

Amefafanua kuwa mwaka 2008 serikali ilijenga jengo la abiria lenye ukubwa wa mita 1500 na mwaka 2012 iliongeza ukubwa wa jengo hilo kutoka mita 1500 hadi mita 2000 na kuwa na uwezo wa kuchukua abiria 48 pekee ambapo kwa sasa linatumika.

Mkurugenzi huyo ameweka wazi kuwa kutokana na ongezeko la abiria wanaoingia na kutoka Mkoani Katavi kwa shughuli za kibiashara na kijamii hususani yaliyochochewa baada ya maboresho yaliyofanywa na serikali kwenye shirika la ndege nchini usafiri wa anga umekuwa kimbilio la watu wengi hivyo jengo hilo kushindwa kukidhi mahitaji.

“Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonyesha ongezeko la watu kuwa ni kubwa ripoti inaonyesha ni watu zaidi ya Milioni 1.152 ni wazi mkoa wa Katavi shughuli za kiuchumi nazo zimeongezeka hivyo kufanya uhitaji wa usafiri wa ndege kuwa mkubwa na kufanya serikali mwaka 2023 ianze ujenzi wa jingo jipya,”amesema Mkurugenzi huyo.

Ujenzi wa jengo hilo jipya la abiria litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 240 kwa wakati mmoja tofauti na ambalo lilikuwa likitumika hapo awali.

Ameongeza “Jengo hili jipya hadi kukamilika na kuanza kutumika fedha zaidi ya Bilioni 1.4 zitatumika ambazo zinajumuisha mifumo yote ikiwemo mifumo ya CCTV, Uzimaji moto, Kuchakata taarifa za abiria wanapoingia kwenye uwanja wa ndege, Sehemu ya kuegesha magari na mifumo mingine inayohitajika kwenye jengo”.

Ameongeza kuwa uwanja huo unapokea ndege za shirika la ndege ATCL zinazokuja na kuondoka katika mkoa huo mara tatu kwa wiki ambapo kila safari ya ndege inabeba abiria wapatao 76 hivyo kurahisisha safari wa anga kwa wakazi wa mkoa wa katavi.

Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema anashukuru kwa taarifa na amewapongeza Kwa kazi nzuri iliyofanyika hapa.

Kwa upande wa wananchi waliohudhuria mapokezi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wamesema kuwa ujenzi wa jingo jipya la abiria ni mwanzo mpya wa mapinduzi wa shirika la ndege kwa Mkoa wa Katavi kwani utasaidia abiria wengi kutumia usafiri huo.

Mkazi wa Kijiji cha Mtisi halmashauri ya wilaya ya Nsimbo Mkoani humo Johnson Malendeja amesema kuwa ndoto ya wananchi wengi hususani wafanyabiara ni kuutumia usafiri wa ndege kwa maendeleo kwenye kukuza biashara zao kwani watakuwa na uwezo wa kusafiri kwa haraka kwenda kununua bidhaa na kurudi.

“Nimefurahi kuona jingo hili jipya abiria ni kweli kazi kubwa imefanyika na baada ya kukamilika fursa kubwa zaidi kwenye sekta ya utalii pia inafunguka kwa haraka maana tunahifadhi ya wanyamapori ambayo inahitaji zaidi wangeni,”amesema Malendeja.

Joyce Peter, Mkazi wa mtaa wa Nsemlwa Manispaa ya Mpanda amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kufanya maboresho katika sekta ya usafiri wa anga ambao umeibadilisha Katavi kiuchumi.

Amebainisha kuwa idadi ya abiria imeongezeka kutokana na Mkoa wa Katavi kuwa niwenye fursa kubwa za kiuchumi pamoja na nauli za usafiri wa anga kuwa nafuu “ Usafiri wa ndege kwa sasa niwakawaida kwa sasa tofauti na hapo awali ulionekana ni wa watu matajiri pekee hii ni kwa sababu Samia wetu anatupenda na amefanya usafiri huu kuwa wa kila mtu”.