*Yashika nafasi ya saba miongoni mwa nchi 18 zilizo bora duniani kwa utalii, Kairika, Dkt. Abbas wafunguka miaka mitatu ya uongozi wake
Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
TANZANIA imekuwa nchi ya saba duniani miongoni mwa nchi 18 zilizo bora kuweza kutembelewa na watalii wengi kwa mwaka jana (2023), ambapo pia mbuga ya Serengeti imeorodheshwa kuwa moja kati ya maeneo maridhawa kabisa ya kutembelea kwa mwaka huo.
Mbunga hiyo ya Serengeti imeshika nafasi ya tatu katika vivutio vya asili duniani mwaka 2023. Mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, wakati akihojiwa katika kipindi cha dakika 365 kinachorushwa na Clouds Media Group, alipokuwa akieleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia.
“Nilisafiri kwenda Japan mwaka jana, sehemu nilipokwenda Wajapani wakataka kujua nchi ninayotoka, nikawaonesha kwenye ramani wakashindwa kuitambua.
Mwaka huu Wajapani walewale waliponiuliza natokea nchi gani, nikawaambia Tanzania, mmoja akafungua ‘iPad’ yake na kusema ‘Royal Tour’, na mimi nikasema, ndio ‘Royal Tour’, yani nchi ninayotoka inaitwa Royal Tour, kwa kweli nilishangaa sana kuona namna gani filamu hii imeitangaza nchi yetu kwa kiasi kikubwa hicho,” amesema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki amesema faida kubwa tuliyonayo kwa sasa ni kwamba tuna Serikali sikivu sana. “Pale tunapokuwa na mapendekezo huwa wanatusikiliza, hivyo tunashukuru sana kwa hilo,alisema Waziri Kairuki.
“Lazima tupongeze maono makubwa ya Royal Tour kwa sababu, Rais Samia aliona mbali sana. Alichokifanya Rais Samia ni kuitangaza Tanzania Duniani, naamini Royal Tour imefungua milango mingi sana kwa Tanzania”.
Amesema ameona vitu vingi sana ambavyo hajawahi kuviona tangu ameanza utaili mwaka 1998.
“Ndani ya hii miaka mitatu ya Rais Samia, juzi hapa nilikuwa Airport, nikakuta tangazo kwenye ‘screen’ linatangaza mbuga inaitwa Chamanyani.
Nikasema hii Mbunga sijawahi kuiona tangu nimeanza utalii hawa wametoka nayo wapi? Hapo ndio nikaanza kuhisi kwamba hii imetokana na chachu ya Royal Tour iliyotokana na Rais Samia ,” amesema Waziri Kairuki.
Amesema wameona mafanikio katika kuvutia wawekezaji hasa katika huduma za malazi.
Aliongeza kwamba katika eneo hilo, ili kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji, kwa mwaka 2023 Wizara ilifanya maboresho ya kanuni za ada na tozo za utalii, ambapo katika maboresho hayo walilenga kupunguza ada katika ya huduma za malazi zinazomilikiwa na Watanzania ili kuwawezesha kuwekeza katika sekta hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, akizungumza kwenye kipindi hicho, amesema;
“Niseme tu ukweli, nilishangaa sana kuona Rais Samia anaigiza filamu halafu yeye mwenyewe ndio ’Sterling’ wa filamu hiyo.
Kwanza kule kuigiza filamu, na yeye kura mhusika mkuu nilijiuliza maswali mengi sana. Kwanza ulinzi wake, location atakazokwenda, wanaomchukua kwenye kamera na muda wake. Kwa kweli nikadhani kwamba hii haitowezekana. Na imenishangaza sana kuona imewezekana.”
Dkt. Abbas amesema kwa upande wa huduma za malazi, kabla ya 2021 tulikuwa na Hoteli 1,818 zenye sifa za kukusanya tozo ya kitanda kwa siku ambapo idadi hiyo imeongezeka kufika 8981 sawa na ongezeko la takribani asilimia 378.3.”
Kwa upande wake mbunge wa Mbunge wa Kawe, Mchungaji Josephat Gwajima, amesema katika kipindi cha mwaka 2021, Rais Samia, alipokuwa akiingia madarakani, Tanzania ilikuwa ikipokea watalii wa nje 922,692 na mapato ya Dola za Kimarekani Bilioni 1.31.
“Lakini 2022 watalii waliongezeka kufika 1,454,920 na kutuingizia kiasi cha dola za Kimarekani Bilioni 2.53. Kwa mwaka 2023, tuliweza kuona ongezeko kubwa zaidi la wageni kutoka nje ambapo ilifikia watalii 1,808,205 ambapo idadi hii iliweza kuingiza kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 3.37,” amesema.
Amesema kupitia filamu ya The Royal Tour, Rais Samia, alifanya mahojiano na majarida makubwa duniani. Alifanya mahojiano ya New York Post, New York Times, The New Yorker na Travel Weekly. Na kutokana na ripoti iliyokuja mwishoni mwa mwaka jana, watu bilioni 1 duniani waliiona Royal Tour au waliisikia”.
Mdau wa Utalii, Timothy Mdinga, amesema kupitia takwimu za Benki Kuu nchini, zinaonesha kwamba Sekta ya Utalii imeweza kuingiza fedha nyingi za kigeni kuliko sekta yeyote ambapo jumla ya Dola za Kimarekani Bilioni 3.37 ambazo sawa na takribani na Trilioni 8 za Kitanzania zimeweza kupatikana ndani ya mwaka 2023 kutoka Januari hadi Desemba.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Misitu (TFS), Dos Santos SIlayo, alisema mafanikio ya Rais Dkt. Samia, ndani ya miaka mitatu kwenye utalii hasa katika sekta ya uwindani ni makubwa sana.
“Mwaka 2021 watalii wawindaji walikuwa 355, lakini muda huu 2024, wako watalii wa uwindaji 787 na hii imetokana na Rais Samia Suluhu kurejesha imani ya watalii hawa nchini, na pia Royal Tour imesaidia sana kufungua nchi,” amesema.
Naye Mdau wa Utalii, Suleiman Masato, amesema mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 2.57 kwa mwaka 2022 hadi kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.37 kwa mwaka 2023 ambapo hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 33.5.
Amesema hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu Afrika nyuma ya Morocco na Mauritius, na ya kumi duniani kwa kuwa na ongezeko kubwa la mapato ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19 mwaka 2019. Hii ni kutokana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) za mwaka 2023.
More Stories
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto