June 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Mwinyi aimwagia sifa Kampuni ya Oryx Gas

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Kampuni ya Oryx Gas kwa kujenga bohari ya kwanza ya kuhifadhi nishati za gesi huku akizitaka kampuni za gesi kuhakikisha wanaweka mikakati itakayowezesha kupungua kwa bei ya gesi ili waipate kwa gharama nafuu.

Akizungumza mbele ya wananchi wa Zanzibar baada ya kuzindua bohari hiyo ya kupokea na kuhifadhi gesi pamoja na miundombinu mingine jumuishi, Dk.Mwinyi amepongeza ujenzi wa bohari hiyo huku akizipongeza taasisi nyingine ambazo zimefanikisha ujenzi wa mindombinu jumuishi ya bandari ya Mangapwani ambayo itahusika na meli za mafuta na gesi pamoja na shughuli nyingine.

“Kwa muda mrefu tulikuwa tunamia bandari ya Malindi lakini kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi bandari ile haitoshi, hivyo Serikali ilitangaza eneo la Mangapwani kuwa bandari kwa ajili ya nishati ya gesi, mafuta na miundombinu mengine.

“Sasa tutakuwa tunapokea meli kubwa na kuhifadhiwa katika matanki mawili makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi tani 130 yaliyojengwa na Oryx. Hivyo niziombe kampuni nyingine kufuata nyayo za Oryx kwa kujenga miundombinu yao katika eneo hili,”alisema.

Pia alisema kuanzishwa kwa bohari ya kuhifadhi ya gesi Zanzibar kutaongeza chachu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na hivyo kufikia malengo ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwamba ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya wananchi itumie nishati safi ya kupikia huku akisisitiza umuhmu wa bei ya gesi kupunguzwa ili wananchi wengi watumie.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Limited, Benoît Araman alisema kufunguliwa kwa bohari ya gesi Mangapwani inanaonyesha dhamira ya Oryx Energies ya kuwekeza katika miundombinu muhimu inayosaidia matumizi salama na mapana ya gesi ya LPG nchini Tanzania.

Pia inakidhi ombi la Serikali la kuhakikisha usambazaji endelevu wa LPG kila mahali nchini.Soko la gesi la Tanzania limeshuhudia ongezeko la uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa karibu mara 13 katika muongo uliopita, kutoka tani 20,000 mwaka 2010 hadi tani 293,000 mwaka 2023.

Aliongeza Oryx Gas Zanzibar imeungana na kampuni ya TP Limited yenye makao yake Zanzibar ambayo ni kampuni tanzu ya Vigor Turky’s Group of Companies (Vigor Group), kujenga bohari hiyo ya kimkakati na kuongeza usambazaji wa gesi ya LPG kisiwani humo.

“Mkataba huu unaonyesha kujitolea kwa Oryx Energies katika kuendeleza ushirikiano na makampuni ya wazawa.Bohari ya Mangapwani, ambayo ilianza kufanya kazi mapema Mei ina uwezo wa kuhifadhi tani 1,300 za gesi ya LPG, na ilipokea meli yake ya kwanza ya tani 1,200 mnamo Mei 2, 2024.

“Pia kusaidia Mpango wa matumizi wa nishati safi ya kupikia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Gesi ya LPG inazidi kuwa sehemu muhimu ya mchanganyiko wa matumizi ya nishati mbalimbali za kupikia Zanzibar, ikishughulikia mahitaji ya kaya, biashara, na sekta ya utalii inayokua kwa kasi,”alisema.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Zanzibar Limited, Shuwekha Omar Khamis alisema: “Tunajivunia kuzindua bohari hii ya kisasa ya LPG ambalo itaimarisha usambazaji wa gesi ya LPG katika visiwa hivyo. Tumedhamiria kuendelea kuchukua jukumu muhimu katika maendeleo haya, kwa kuwa tumeweka msingi wa kupanua usambazaji wa LPG Zanzibar.

Awali Mwenyekiti wa kampuni za Vigor Toufiq Salim Turky alisema wameungana Oryx kwasababu ya kutambua uwezo wao wa miaka mingi katika soko la gesi nchini , hivyo ni imani yao sasa gesi itapatikana kwa wengi.

Pia alisema mpango wao ni kupunguza bei ya gesi Zanzibar kwa asilimia 20 kuanzia Julai 1 mwaka huu na baadae kupungua bei kwa asilimia 30. “Hivyo Oryx Gas wameiweka bohari hii katika viwango vya kimataifa, tunafahamu wao wako kwa miaka mingi, wana uzoefu mkubwa.

“Bohari hii inamilikiwa na Vigor kwa asilimia 100, lakini kwa uendeshaji tumamua kuwapa wenzetu wa Oryx .Uendeshaji tumeukabidhi kwa Oryx kwa kuamini wao ni kinara katika soko la Tanzania.Wakati tunaanza huko nyuma soko lilikuwa ni tani tatu lakini sasa soko lao limekuwa na kufikia tani 800,”alisema.

Kwa upande wake wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar(ZURA), Omar Ali Yussuf alisema kwa miaka mingi sekta ya nishati hasa gesi, walikuwa wanatumia bandari ya malindi lakini sasa wamepeta bandari ambayo itashusha gesi, mafuta na itatumika kwa shughuli nyingine kwenye hilo la Mangapwani.

“Kabla ya kuwepo kwa bandari hii ya kushusha gesi na mafuta tulikuwa tunatumia majahazi na vyombo vingine ambavyo havina salama lakini kwa maelekezo ya Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi leo tumeweza kuwa na bandari kwa ajili ya meli zenye gesi na mafuta,”alisema.

Pia alisema kwa kupitia mipango ya Serikali pamoja na sera nzuri za uchumi wa bluu watahakikisha bandari ya Mangapwani wanataka iwe kituo kikuu cha kusafirisha gesi na mafuta kwa ukanda wa Afrika Mashariki huku akifafanua kuwa bei ya nishati ya mafuta na gesi kwa Zanzibar iko chini ukilinganisha nchi nyingine.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Limited, Benoît Araman akitoa maelezo wakati wa hafla ya uzinduzi wa wa bohari ya kuhifadhi nishati za gesi ya Kampuni ya Oryx leo Juni 27, 2024 Visiwani Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akipanda baada ya kuzindua bohari ya kuhifadhi nishati ya gesi ya Kampuni ya Oryx uliofanyika leo Juni 27, 2024 huko Mangapwani Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akikata utepe kuweka jiwe la msingi kuzindua bohari ya kuhifadhi nishati ya gesi ya Kampuni ya Oryx uliofanyika leo Juni 27, 2024 huko Mangapwani Zanzibar.