Wataalamu wawaonya watumiaji wa mitandao ya umma
Na Ismail Mayumba
KATIKA ulimwengu wa sasa wa kidigitali, upatikanaji wa mtandao umekuwa ni hitaji la kila siku kwa watu wa rika zote. Hali hii imefanya maeneo mengi ya umma kama hospitali, vituo vya mabasi, fukwe za bahari, migahawa, maduka makubwa (supermarket), na hata kumbi za starehe na mikutano kutoa huduma ya WiFi bure kwa wananchi. Ingawa huduma hii inaonekana kuwa neema kwa wengi hasa kutokana na kupanda kwa gharama za vifurushi vya intaneti – wataalamu wa masuala ya usalama wa mitandao wameeleza kuwa WiFi za bure ni hatari kubwa kwa usalama wa taarifa binafsi na kifedha. Katika mahojiano maalum na gazeti hili, wataalamu wa
masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) wameonya kuwa watu wengi hutumia WiFi za bure bila kufahamu kuwa wanafungua mlango kwa wadukuzi na wahalifu wa mtandaoni wanaoweza kuiba taarifa zao muhimu kama nambari za kadi za benki, nywila (passwords), na hata picha binafsi.
HATARI ZINAZOJIFICHA KWENYE WIFI ZA BURE
- Shambulio la Mtu wa Kati (Man in the Middle Attack)
Mojawapo ya mbinu maarufu inayotumiwa na wadukuzi ni kujipenyeza kati ya mtumiaji na mtandao. Katika hali hii, kila unachofanya kwenye mtandao – kuanzia kuingia kwenye akaunti zako za benki, barua pepe hadi
mitandao ya kijamii – kinaweza kusomwa na kudukuliwa bila wewe kujua.Hali hii huwafanya wahalifu kupata taarifa zako nyeti kwa urahisi. - Kusambazwa kwa Virusi vya Mtandao
WiFi isiyo salama inaweza kuwa chombo cha kueneza virusi vya kimtandao. Mdukuzi anaweza kutuma irusi kwenye mtandao na mara moja vikaanza kuingia kwenye simu au kompyuta za watumiaji wengine waliounganishwa. Hii inaweza kusababisha kifaa chako kuwa na matatizo ya kiufundi, kupoteza data au hata kudukuliwa. - Mtandao Feki (Fake Hotspot)
Katika mbinu hii, mdukuzi huwasha WiFi yake binafsi na kuipa jina linalofanana na lile la eneo halisi. Kwa mfano, ukiwa kwenye tamasha la “Samia Strength Festival”, unaweza kuona WiFi inayoitwa “Samia Festival” na kujiunga bila kujua ni ya mdukuzi. Mara tu unapojiunga, anakusanya taarifa zako zote, ikiwa ni
pamoja na akaunti zako nyeti. - Udukuzi wa App za Kibenki
Wadukuzi mahiri wanaweza kuingilia moja kwa moja programu zako za kibenki kwenye simu endapo uko kwenye WiFi isiyo salama. Matokeo yake ni kupoteza fedha zako zote bila dalili yoyote ya tahadhari.
TAHADHARI ZA KUCHUKUA KABLA YA KUTUMIA WIFI YA BURE.
Kwa mujibu wa wataalamu, si kosa kutumia WiFi ya bure, lakini ni muhimu kuchukua tahadhari kali ili kulinda usalama wa taarifa zako binafsi. Hapa kuna mbinu salama za kutumia huduma hii bila kudhurika:
- Epuka Kuingia Katika Akaunti Nyeti Usiingie kwenye akaunti za benki au mitandao ya kijamii unapokuwa kwenye WiFi ya bure. Hii ni kwa sababu taarifa zako zinaweza kunaswa na mdukuzi bila wewe kujua.
- Tumia Anti-Virus Bora Programu ya anti-virus iliyosasishwa inaweza kusaidia kukukinga dhidi ya virusi vinavyoenezwa kupitia WiFi ya bure.
- Hakikisha Tovuti Unazotembelea Zina “HTTPS” Tovuti zenye “HTTPS” zina usalama zaidi ikilinganishwa na zile zilizo na “HTTP” pekee. Usitembelee tovuti zisizo salama kwani ni rahisi kuibiwa taarifa zako.
WiFi ya bure inaweza kuwa msaada mkubwa kwa wengi hasa katika nyakati hizi ambapo gharama za kuperuzi ziko juu, lakini ni muhimu kuwa makini. Huduma hii siyo bure kama inavyoonekana – gharama
yake inaweza kuwa usalama wako binafsi. Kwa hiyo, kabla hujajiunga na WiFi ya bure popote pale, jiulize: “Je, ni salama kweli?” Kwa usalama zaidi, tumia intaneti ya kibinafsi au hakikisha una VPN, anti-virus, na unazifahamu tovuti salama. Lakini kama unaweza, epuka kabisa kutumia WiFi za bure –ni heri kutumia kidogo chako kuliko kupoteza kikubwa chako - Tumia VPN (Virtual Private Network). VPN huficha utambulisho wako wa mtandaoni na kufanya taarifa zako zisomeke kirahisi na wadukuzi.Ni kinga bora dhidi ya mashambulizi ya mtu wa kati na mitandao feki.
More Stories
Sekta ya madini yakusanya zaidi ya bil.900 hadi kufikia leo
WCF yawataka waajiri kutekeleza wajibu wao
Airtel yazindua tena maduka mapya Dar