Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Mbeya
FALSAFA ya R4 ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetajwa kutumika kuachiwa mapema bila kuumizwa viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wakishikiliwa na Polisi mkoani Mbeya.
Akizungumza jana Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) mkoani Mbeya, Elisha Chonya, alisema waliokuwa wamekamatwa katika kituo walichokuwa wamewekwa makada takribani 54 ni mmoja pekee aliyeumizwa na kupelekwa kituo cha afya kwa matibabu.
“Hadi sasa sijapewa taarifa za jumla lakini kwa waliokuwa kituoni nilipokuwa tulikuwa 54, tupo salama na vifaa vyetu tumepewa isipokuwa mtu mmoja ndiye aliumizwa na kupelekwa hospitali,” alisema Chonya
Mmoja wa makada wa CHADEMA akizungumza kwa sharti la kutotaja jina lake, alisema tafsiri ya falsafa ya R4 za Rais Samia za maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya zimekuwa kauli mbiu ambazo zimesaidia kumaliza haraka sakata baina ya viongozi na wafuasi wa CHEDAMA waliokuwa wamekamatwa na Polisi na kila mmoja kusafirishwa kurudishwa alikokuwa ametoka.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kuachiwa na kusafirishwa chini ya ulinzi watu hao hadi maeneo walikotoka.
Jeshi hilo limesema iwapo kuna mtu aliyekuwa ameshikiliwa na hajulikani alipo, familia zao ziulizwe kwa kuwa kila mmoja aliachiwa kwa utaratibu wake ikiwamo baadhi kuachiwa huru na wengine kwa dhamana.
Kuachiwa kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kumethibitishwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Awadh Juma Haji, alipokuwa akizungumza kuhusu watuhumiwa hao waliokamatwa juzi.
Viongozi walioachiwa na kusindikizwa chini ya ulinzi wa Polisi hadi maeneo walikotoka ni Pamoja na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu .
Lissu, Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho, John Pambalu na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na wanachama wapatao 520 ni miongoni mwa waliotiwa mbaroni na Polisi juzi, baada ya kukaidi amri ya Polisi la kutakiwa kutofanya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kutokana na kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Mbali na wanasiasa hao wengine waliokamatwa ni waandishi wa habari, Ramadhan Hamis, Fadhili Kirundwa wa Jambo TV pamoja na Francis Simba ambaye ni mpigapicha wa Chanzo TV waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ofisi za kanda ya Nyasa, jijini Mbeya.
Wanahabari hao walikamatwa kunatokana na uamuzi wa kuelekea jijini Mbeya kushiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyopangwa kufanywa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).
Kamishna Haji alitangaza kuachiwa kwa baadhi na ambao hawakuachiwa ni wale walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana na kuwa na makosa zaidi ya moja ikiwamo jinai na kwamba jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akitumia ukurasa wake wa kijamii aliandika kwamba; “Viongozi wakuu wa CHADEMA Freeman Mbowe, Tundu Lissu, John Mnyika, Pambalu wamerejeshwa Dar es Salaam na Polisi na wamejidhamini wenyewe.
Aidha, alisema kuna taarifa za baadhi ya viongozi wa BAVICHA kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mbeya, ambapo aliahidi kutoa taarifa baadaye.
Hata hivyo, Kamishna Haji, akizungumza na mtandao mmoja wa kijamii alisema waliokuwa wamekamatwa kwa kukaidi agizo la jeshi kuhusu kongamano la vijana, wote waliruhusiwa.
“Huyo anayesemwa hajulikani alipo aulize familia yake, wote waliokuwa wamekamatwa kama nilivyoeleza katika mkutano na waandishi wa habari, wameruhusiwa na kusindikizwa na polisi wakiwa salama,” alisema Haji.
Alifafanua kuwa hadi sasa hana taarifa zozote za kushikiliwa mtu yeyote kufuatia taratibu zote za dhamana kukamilika kwa waliokuwa na makosa zaidi ya moja kama ilivyoelezwa hapo awali.
“Waliokuwa na makosa zaidi ya moja wote walikamilisha taratibu za dhamana, hivyo hadi sasa sina taarifa za kukamatwa kwa mtu yeyote, kila mmoja aliachiwa kupelekwa kwake,” alisema kamishna huyo.
Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Elisha Chonya alisema waliokuwa wamekamatwa katika kituo walichokuwa wamewekwa makada takribani 54 ni mmoja pekee aliyeumizwa na kupelekwa kituo cha afya kwa matibabu.
Alisema walipelekwa kituo cha kati tukiwa viongozi kama wanne, mwenyekiti wa chama mkoa Masaka Caroli, katibu mkuu Gwamaka Mbugi, Hamad Mbeale na katibu mwenezi, Twaha Mwaipaya, ambaye baadaye aliondoshwa kupelekwa sehemu nyingine,” alisema.
“Hadi sasa sijapewa taarifa za jumla lakini kwa waliokuwa kituoni hapo, tupo salama na vifaa vyetu tumepewa isipokuwa mtu mmoja ndiye aliumizwa na kupelekwa hospitali,” alisema Chonya.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato