Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline.
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imethibitisha kuwa iko mbioni kusaini makubaliano ya awali na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Institute-DMI) yenye lengo la kushirikiana kuanzisha kituo chenye ithibati na kinachotambulika duniani kitakachokuwa kinatoa mafunzo ya masuala ya usalama baharini.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Charles Nyangi, kwenye mjadala uliofanyika katika Kongamano la Nishati na Viwanda uliofanyika Zanzibar, ambapo amesema kuwa moja ya mikakati inayoendelea kutekelezwa na Mamlaka hiyo ni pamoja na utatuzi wa changamoto ya ukosevu wa vyeti na elimu ya masuala ya usalama baharini.
Nyangi amesema, ukosefu wa vitu hivyo ni jambo ambalo limekuwa likidumaza ushiriki wa watanzania kwenye miradi ya utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia nchini, hususan katika miradi inayotekelezwa katika maeneo ya baharini, huku akibainisha kuwa ukosefu wa vyeti ni moja ya changamoto kubwa kwani huzuia watanzania wenye ujuzi stahiki kushiriki kwenye miradi ya mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini.
“Kwa sasa hakuna Kituo chenye ithibati nchini, kinachotoa kozi za masuala ya usalama na tahadhari kama vile Basic Offshore Safety Induction And Emergency Training (BOSIET) inayowezesha mtu kupata kibali cha kufanya kazi katika miradi ya mafuta na gesi inayotekelezwa baharini,
“Changamoto hii imesababisha watanzania wenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi kwenye miradi hiyo kulazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa kusomea kozi hizo..kwakweli hii ni changamoto kwa ni watanzania wachache wanaoweza kumudu gharama hizo”,amesema Nyangi.
Aidha Nyangi ameongeza kuwa, kuanzishwa kwa Kituo hicho nchini kutawezesha watanzania wengi kupata cheti Cha Usalama na umahiri baharini, hivyo kutasaidia ongezeko la watanzania kushiriki katika miradi ya mafuta na gesi asilia hususan miradi ya Mkondo wa Juu wa Petroli inayotekelezwa nchini.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato