Na Penina Malundo, timesmajira, Online
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imesema vikwazo vyovyote katika uzalishaji wa Mradi wa Kuchataka Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) katika Mkoa wa Lindi unaotarajia kuanza mwaka 2025.
Pia imesema hadi sasa tayari makubaliano ya awali ya mkataba husika yamefanyika ikiwemo majadiliano ya muundo wa mradi, ukubwa wa mradi, sheria iweje na kwamba majadiliano yakikamilika wanatarajia Desemba 8 mwaka huu kusaini mkataba uliokamilika.
Ameyasema hayo jana Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya 46 maarufu Sabasaba yanayofanyika katika Kiwanja cha Mwalimu Julius Nyerere Temeke Dar es Salaam.
Sangweni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Majadiliano hayo amesema baada ya mkataba rasmi kukamilika wanatarajia kwenda kwenye kazi ya usanifu wa mradi na namna ya kupata fedha za utekelezaji.
“Tunategemea utekelezaji wa mradi huu ujenzi uanze mwaka 2025 na ndani ya miaka minne hadi mitano utakuwa umekamilika na gesi ya kwanza itaanza kutoka 2030,” amesema.
Amesema endapo hakutakuwa na changamoto katika mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh.trilioni 70 utaweza kuzalisha gesi asilia kwa miaka 30.
Mhandisi Sangweni amesema tafiti zinaonesha kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa kama hiyo ikifanyika katika nchi kama Tanzania pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1.5.
“Huu sio mradi mdogo, wakubeza, kwani utachangia ukuaji wa uchumi kwa kasi kubwa na pato la taifa litaongezeka kwa asilimia 1.5, ndio maana timu ya Serikali hailali kuhakikisha mradi unatekelezwa,” amesema na kuongeza
“Baada ya mradi huo kuanza kuzalisha gesi asilia wanatarajia kuuza katika nchi za Mashariki ya Mbali kama Japani, China na nyinginezo ambazo zimeonekana kuhitaji,”amesema
Amesema wawekezaji wa Kitanzania na wengine kujipanga vizuri katika kutumia fursa zitakazokuwepo katika mradi huo, akitolea mfano kuwa nondo, saruji na bidhaa nyingine zitahitajika.
“Tumekuwa tukifanya mikutano na wadau mbalimbali kama wakuu wa taasisi waweze kujiandaa kushiriki katika mradi huo ambao unaenda kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo,”amesema na kuomgeza
“Katika kipindi cha ujenzi wa mradi huo zaidi ya ajira 10,000 zitapatikana na ajira za kudumu zitakuwa zaidi 600 pamoja na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi kwenye eneo la mradi,”amesema
Amesema kazi ya PURA ni kushauri Serikali kuhusu shughuli za mkondo wa juu, kuthibiti na kusimamia Mradi wa LNG ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania.
“Watanzania karibuni katika banda la PURA kuja kutembelea na kujifunza kazi zinazofanywa na taasisi yetu na kutumia fursa katika miradi mbalimbali inayosimamia,”amesema
More Stories
Tanga kutumia vituo 5405,kupiga kura leo
NMB yatoa msaada wa vifaa Mufindi
Viongozi wa dini Katavi waomba wananchi kujitokeza kupiga kura