NA MWANDISHI WETU, ARUSHA.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) tayari umewalipa wanachama 750 waliokumbwa na sakata la vyeti “feki”, baada ya kuwasilisha madai yao na nyaraka stahiki.
Akizungumza wakati wa kikao kazi na wanachama wapatao 60 wa klabu ya waandishi wa habari jiji la Arusha kwenye ukumbi wa Kituo Cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) leo Ijumaa Desemba 2, 2022, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama PSSSF, Bw. James Mlowe amesema, zoezi la kuwalipa lilianza Novemba 1, 2022 na ni endelevu.
“Zoezi linaendelea vizuri, Wanachama waliopo katika orodha ya serikali na PSSSF ni 9,771 ambao wanadai malipo ya takribani shilingi bilioni 22.22.” Alifafanua.
Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho na wanachama wa klabu hiyo ya waandishi wa habari jijini Arusha wapatao 60, Bw. Mlowe alisema “lengo ni kutoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko pamoja na kuendeleza uhusiano mzuri ukiopo kati ya Mfuko na wanahabari wa Arusha”.
Mambo mengine aliyozungumzia Bw. Mlowe ni pamoja na Malipo ya Mafao na Pensheni, Uwekezaji, Thamani ya Mfuko pamoja na mafanikio ambayo PSSSF imeyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 baada ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF, PPF,LAPF na GEPF.
“ Kila mwezi PSSSF inaingiza kwenye mzunguko zaidi ya shilingi bilioni 180 ikijumuisha malipo ya pensheni ya mwezi zaidi ya shilingi bilioni 60 zinazolipwa kwa wastaafu 158,000 pamoja na Mafao mengine zaidi ya shilingi bilioni 120,” alibainisha.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanachama wa klabu hiyo, Katibu wa klabu hiyo, Bw. Seif alisema wanashukuru kwa fursa hii na wameweza kufahamu kwa undani juu ya PSSSF na utekelezaji wa majukumu yake na sasa wanaweza kutoa taarifa sahihi na muhimu kwa wadau wa PSSSF.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti