January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSF Kigoma yapigwa marufuku uendelezaji ujenzi eneo la ukanda wa kijani

Na mwandishi wetu, TimesMajira Online, Kigoma

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amepiga marufuku Shirika la Mafao ya Wastaafu Nchini PSSF kuacha mara moja uendelezaji wa Jengo lao katika Manispaa ya Kigoma kutokana na Shirika hilo kupewa eneo lililoifadhiwa kwa ajili ukanda wa kijani.

Waziri Silaa amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kusimamisha maendeleo yoyote ya ujenzi katika eneo hilo ikiwemo Ofisi ya Mtendaji Kata pamoja na kuondelewa kwa shughuli nyingine za kijamii na wafanyabiashara ndogondogo.

Waziri Silaa alisema hayo wakati akihitimisha ziara yake siku mbili mkoani Kigoma na kuwataka watendaji wote wa sekta ya ardhi Mkoani humo kuzingatia matakwa ya sheria za ardhi ili kila mtu apewe haki yake wakati wa kufuata taratibu za kumiliki ardhi.

Waziri Silaa alisisitiza kuwa suala PSSF haliitaji hata yeye kurudi Ofisini bali hataki kabisa na hivyo kumuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma kutoa taarifa kwa viongozi wa Shirika hilo kutafuta eneo lingine hta kama linahitaji kutolewa fidia akiongeza kuwa Shirika hilo ni kubwa.

Agizo la Waziri Silaa pia likawaangazia pia watu wa takwimu ambao pia wametwaa eneo bila kuwa na hati milki ya eneo husika nakuagiza waandikiwe barua ili viongozi wao wajue kuwa walinunua eneo bila kuwa na hati.

‘’Kama mmegawa eneo lililoifadhiwa kwa namna yoyote mkagawa ofisi ya Kata, hiyo ofisi ya Kata itavunjwa alafu mtamweleza Waziri wa TAMISEMI kwanini fedha zake zimetumika kujenga katika eneo ambalo sio sahihi kwa matumizi yale ndio maana nakataa mabadiliko ya matumizi ya viwanja.’’Aliongeza Jerry Silaa Waziri wa Ardhi.

Waziri Silaa aliongeza kuwa kama wataalamu wa ardhi wanataka kubadilisha matumizi ya ardhi katika eneo fulani ni vyema wakishirikisha wananchi ili makubaliano yafanyike kwa pamoja ili kila mtu aelewe kusudio hilo kwani wananchi hao pia wana haki ya kupendekeza matumizi wayatakayo.

Waziri Silaa amehitimisha ziara yake mkoani Kigoma na anaendelea na ziara nyingine kama hiyo mkoani Katavi ambapo ataendelea kujionea shughuli mbalimbali mkoani humo ikiwemo utoaji hati kwa wananchi waliokamilisha taratibu za utwaaji ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maeneleo ya Makazi Jerry Silaa akipitia nyaraka mbalimbali wakati wakushughulikia mgogoro wa Ardhi jana katika Manispaa ya Kigoma.
Baadhi ya wananchi wakishuhudia Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa alipofika uwandani kusikiliza utatuzi wa mgogoro wa kiwanja.