November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSPTB yazindua wimbo maalum

Na Penina Malundo

BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini Tanzania (PSPTB), imezindua rasmi wimbo maalum wenye lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na bodi hiyo.

Akizindua wimbo huo leo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya maonesho ya 44 ya biashara ya kimataifa maarufu kama sabasaba, Kaimu Mkurugenzi wa bodi hiyo, Godfred Mbanyi amesema, wimbo huo umeweka msisitizo katika suala la usajili ambao kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha bodi hiyo ya wataalamu wote wa ununuzi na ugavi wanatakiwa wawe wamesajiliwa na bodi ndipo waweze kufanya kazi za ununuzi.

Amesema, ni kosa la kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 11cha sheria namba 23 ya mwaka 2007 iliyoanzisha bodi hiyo ni kosa kwa mtu yeyote kufanya kazi ya ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na bodi.

“Wimbo huo utaweka msisitizo katika jambo hilo lakini pia utaelezea kazi mbalimbali za bodi kama kuwahimiza watu kuja kufanya mtihani ili waweze kuwa na sifa za juu za taaluma za ununuzi na ugavi,” amesema

Aidha amesema, katika wimbo huo umeweka kutangaza kazi za ushauri wanazozitoa na mafunzo mahususi ya taasisi za serikali na Binafsi .

“Katika wimbo huo tumeelezea mafanikio tuliyopata na kuonyesha taasisi ambazo wameweza kuzitolea mafunzo yaliyowasaidia kufanya vizuri katika eneo la manunuzi,” amesema

Ametoa wito kwa wataalamu waliopo vyuoni na makazini wajikite katika suala la usajili na wasisahau kupandishwa madaraja wasipofanya mitihani ya bodi ili waweze kupata sifa.