Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu amewataka waganga wafawidhi kuhakikisha dawa ya selimundu (hydroxyurea) inapatikana katika vituo vyote vya afya ili kubadilisha maisha ya watoto wenye ugonjwa huo.
Prof. Nagu ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es salaam wakati akizingumza na waandishi wa Habari katika Kongamano la kisayansi kuhusu ugonjwa wa selimundu ambalo limejumuisha nchi mbalimbali Duniani lenye maudhui ya kuzindua jarida mahususi kwaajili ya ugonjwa wa selimundu na kujadili mbinu ambazo zitaweza kupunguza tatizo hilo ulimwenguni.
“Dawa Moja ambayo inabadilisha maisha ya watoto wenye selimundu ni hydroxyurea ambayo inapatikana Tanzania na bohari yetu ya Taifa inayo wakati wote, na tunaendelea kuhakikisha kwamba dawa hii inatengenezwa hapa nchini ambapo itatusaidia kupunguza gharama na kuhakikisha unakuwepo wakati wote”
“Serikali imetenga fedha kwaajili ya kuhakikisha wagonjwa wa selimundu wanapata dawa ya selimundu (hydroxyurea) na dawa hii ipo kwenye miongozo ya dawa” Amesema Prof. Nagu
Aidha pamoja na takwimu kuonesha Tanzania jumla ya watoto 11,000 hadi 14, 000 kila mwaka wanazaliwa na ugonjwa wa selimundu Serikali imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na tatizo hilo kwa kuutambua ugonjwa mapema, kuhakikisha matibabu yanakuwa mazuri na Bora lakini pia upatikanaji wa dawa.
“Ugonjwa wa selimundu unaathiri watoto na watoto hawa huwa wanaugua mara kwa mara, wanaongezewa damu, wanakosa shule na wakiwesa kuishi mpaka ukubwani wanakosa pia kazi”
“Serikali imejitahidi kuhakikisha kwamba utambuzi wa ugonjwa huu upo kwenye hospitali zote 7 za rufaa za kanda, hii ni kulinganisha na mwaka 2015 ambapo ni hospitali Moja tu ya muhimbili ndiyo ilikuwa na uwezo wa kugundua ugonjwa huo, hii ni hatua kubwa sana serikali imefanya” Amesema Prof. Nagu.
Pia serikali imehakikisha matibabu ya watoto wenye selimundu yanakuwa mazuri na Bora ambapo imetoa mungozo wa matibabu ambao unaainisha nyanja zote kuanzia kupunguza tatizo hilo hadi kuhakikisha kwamba wanafanyiwa matibabu.
“Muongozo huu utasaidia kuhakikisha kwamba watoa huduma wetu wanajua nini chakufanya wakati gani na kwahivyo kufanya kwa usahihi na kupelekea kuboresha matibabu ya watoto hao”.
Juhudi nyingine ambayo serikali imeifanya ni matibabu ya upandikizaji uloto ambayo inapunguza sana tatizo la selimundu.
Prof. Nagu amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa bajeti ya mwaka 2023/24 kwa kutenga Bilioni 5 kwaajili ya upandikizaji ambapo kwa sehemu kubwa itatumika kupandikiza uloto .
Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema wao kama chuo kikuu wanaendelea na ufanyaji tafiti za kuzuia, kuchunguza, upandikizaji uloto na kutibu ugonjwa wa selimundu ambapo wanashirikiana na mataifa mbalimbali kama vile marekani na ulaya kisha kuleta majibu na Mapendekezo ya tafiti hizo.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa