January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo:Maendeleo Jimbo la Musoma Vijijini yataendelea kuwa shirikishi

Fresha Kinasa, TimesMajiraOnline,Mara

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara Prof.Sospter Muhongo amesema kuwa,suala la maendeleo ndani ya Jimbo hilo litaendelea kuwa  shirikishi kwa Vijiji, Vitongoji na kata zote kwa ajili ya manufaa ya Jamii.

Ameyasema hayo Novemba 28,2024 wakati akielezea utekelezaji wa maendeleo jimboni humo pamoja na kueleza matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.

“Jimbo la Musoma Vijijini lina jumla ya
Kata 21,Vijiji 68 na Vitongoji 374, Ambapo Vijiji 66 imeshinda CCM,   
Vijiji 2,CHADEMA na ushindi wa CCM ni  97.06%. Upande wa ushindi wa  Vitongoji CCM  imeshinda Vitongoji 357, na Vitongoji 17,CHADEMA,Ushindi wa CCM ni 95.45%”ameeleza Prof. Muhongo kupitia taarifa yake na kuongeza.

“Matokeo ni hayo,Tusisahau kwamba sisi Musoma Vijijini huwa hatuna ubaguzi wa kisiasa na hatuna ubaguzi wa aina yoyote ile!. Muhimu kwetu ni maendeleo shirikishi kwa manufaa ya jamii yote ndani ya vitongoji, vijiji na kata zetu zote.” amesema Prof. Muhongo.

Aidha ameeleza kuwa,”Kuanzia wiki ijayo tunaendelea na utekelezaji wa miradi yetu iliyobuniwa na kuanza kutekelezwa kwa kutumia nguvu za wanavijiji. Baadhi ya miradi hiyo imeanza kupata michango ya fedha kutoka Serikalini.”

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni  mingi, ambapo  baadhi yake ni ujenzi wa maabara tatu (3) za masomo ya sayansi kwa kila sekondari ya Kata, ujenzi wa sekondari mpya kumi (10), ujenzi wa shule shikizi nane (8) mpya na ujenzi wa zahanati mpya (17).

Shadrack Bwire ni Mkazi wa Kata ya Etaro Jimbo la Musoma Vijijini akizungumza na Times Majira amesema, ili kujiletea maendeleo ni wajibu wa Wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali.  Huku pia akipongeza jinsi Mbunge wa Jimbo hilo ambavyo amezidi kuwaleta pamoja Wananchi katika shughuli za  ujenzi wa miradi ya  maendeleo jimboni humo.