January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mkumbo: Hakuna suala la mauzo ya Bandari

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo amesema makubaliano yalihusu Bandari ni uendelezaji na uboreshaji na sio uuzwaji wa bandari kwani kwa sasa kinachozungumziwa ni uboreshwaji wa magati saba kama gati la magari, gati la mizigo mchanganyiko, gati la makontena, gati la majahazi na abiria, n.k.

Aidha amesema kampuni ya DP World ikija lazima isajiliwe Tanzania kwa kufuata sheria zote za Tanzania. Hata bila mkataba, endapo kutatokea tatizo basi sheria za Tanzania zitachukua hatua.

Mbunge Mkumbo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizingumza na waandishi pamoja na wahariri wa vyombo vya Habari wakati wa Mjadala wa kitaifa wa kulinda na kuendeleza umoja wa kitaifa.

“Hoja za majadiliano ya mkataba wa bandari zimejadiliwa kwa kina na watu wenye uzoefu mkubwa, hivyo kamwe wabunge wasingeingia mkenge kwa kupitisha kitu kisichokuwa na tija kwa Taifa. Watanzania wana hofu na mali zao, ni jambo jema kwao. Tanzania ipo sheria kuwa mikataba ikisainiwa inaweza kuletwa ili kuipitia kwa kina kwa manufaa ya Taifa,” Alisema Mbunge wa Ubungo Kitila Mkumbo.

“Kwenye mambo ya mikataba ya uwekezaji kuna mambo matatu muhimu ambayo wabunge tuliyaangalia na sio hili la mauziano kama inavyosemwa mtaani ila uendelezaji na uboreshaji ambao kwetu ndio kitu muhimu tulichoangalia. Hivyo niseme hapa kuwa yaliyojadiliwa bungeni ni makubaliano sio mauziano,”ameongeza.

Kuhusu Ajira Bandarini, Mkumbo alisema Watanzania na wote wanaofanya kazi bandarini wataangaliwa kwa kina juu ya ajira zao kwani Kama viongozi wana dhamana ya kitaifa ya kulinda, amani, umoja na mshikamano kama nchi.

“Kwenye huu mkataba wa Bandari, wabunge wamechagua uzalendo wa kiuchumi ili kuleta tija kwenye uzalishaji, kodi, ajira na maendeleo ya Taifa kwa ujumla,”

“Kitendea kazi cha mbunge ni hisia na maoni ya Watanzania ili kuangalia tija kwa nchi yetu. Maeneo ambayo yamejadiliwa na Watanzania nje ya Bunge, kabla ya mkataba kupitishwa, yataangaliwa kwa kina. Watanzania na wote wanaofanya kazi bandarini wataangaliwa kwa kina juu ya ajira zao. Kama viongozi tuna dhamana ya kitaifa ya kulinda, amani, umoja na mshikamano kama nchi,”Amesema Mbunge Mkumbo.

Kadhalika Mkumbo amewataka wananchi na wanasiasa kuepuka kuchangia hoja kwa ubaguzi.

“Nchi yetu ina dini na makabila lakini hayo tulikubaliana kuyaepuka kwa manufaa ya nchi yetu. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina pande mbili ambazo ni kitu kimoja. Viongozi wasihukumiwe kwa sababu ya tofauti zao za dini, ukabila, ukanda na rangi. Kwenye uwekezaji kuna mbinu mbili ambazo ni uzalendo wa kiuchumi na uchumi wa kizalendo,”

Kwa upande wake mfanyabiashara Rostam Aziz amesema suala la ushabiki wa kisiasa unaharibu Mjadala wa Bandari.

“Naunga mkono mijadala. Lakini kwenye hili mjadala wa kiuchumi, mjadala wa kibiashara umegeuzwa kuwa mjadala wa kisiasa, kidini na ukabila. Mjadala umekua na ushabiki zaidi badala ya kutaka kujua ishu ni nini.” Amesema Rostam Aziz

Kuhusu umoja wa Kitaifa kwa ujumla , Rostam aliendelea kutetea kwa kusema;

“Nchi yetu ina bahati sana. Ni kisiwa cha amani katika eneo lenye migogoro mingi. Lazima tuwashukuru waasisi wetu ambao wametubeba mpaka leo tupo salama salmini. Leo hii mtu haulizwi ni dini gani wala kabila gani.” Mfanyabiashara Rostam Aziz

Kwa upande wake Godbles Lema alisema Sio dhambi kuleta mwekezaji katika nchi na huwezi kumkwepa kwani Dunia yote inafanya kazi na makampuni makubwa ya kimataifaPia Lema aliongeza kwamba

“Mimi ushauri wangu, Nchi hii inahitaji muwekezaji zaidi ya bandarini.Naye Zitto Kabwe alisema ; “Tofauti ya rasilimali bandari na rasilimali dhahabu, ni kwamba dhahabu unaichimba, ikiondoka ndio imeondoka. Bandari huwezi kuiondoa, ndio maana hata huo mjadala wa kuuza nashangaa mzee (Wasira) ulishtuka. Hata ukiuza utaibeba? Utaipeleka wapi?” Zitto Kabwe.

Kwa upande wake Mwanasiasa Mkongwe Steven Waisara alisema ni vyema kuendelea kuwasaidia watanzania waelewe kuhusu Bandari

“Ni vyema Watanzania wakaendelea kusaidiwa kuelewa uwekezaji unaotarajiwa kufanyika katika bandari zetu, mitandao ilipotosha sana kuhusu suala hilo hasa kwa kuandika uongo kwamba bandari zetu zimeuzwa.”

Mzee Wasira amesema Watanzania waeleweshwe kwamba bandari zetu haziwezi kuuzwa bali kinachofanyika ni miradi ya uwekezaji inayosimamiwa na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania.