November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Viwanda na Biashara ,Prof,Kitila Mkumbo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani)wakati wa ziara ya Kikazi katika Ofisi za Brela ambapo amejionea namna taasisi hii inavyotekeleza majukumu yake.

Prof.Mkumbo ataka migogoro ya kampuni itatuliwe kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

WAZIRI wa Viwanda na Biashara ,Prof,Kitila Mkumbo amesema migogoro ya kampuni inapaswa itatuliwe kwa kufuata misingi ya taratibu ,sheria na kanuni.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi katika Taasisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela),Prof.Kitila amesema kama migogoro hiyo itakuwa mahakamani inapaswa kuiachia mahakama kufanya maamuzi yake na sio kuingilia kwenye maamuzi haya  hadi itakapokamilika.

“Unaweza kukuta kwenye kampuni wamegombana kutokana na hisa au mmoja anataka kuzidisha hisa kwenye kampuni kinyemela haya,yatatuliwe kisheria na kikanuni au  kutumia busara sana ili kuweze kupunguza migogoro mingi,”amesema Prof.Kitila

Aidha Prof.Kitila ametoa wito kwa wafanyabiashara kuwa na muamko wa kusajili biashara  kwa sababu kurasimisha biashara inaanza kwa kusajili.

“Watanzania na wafanyabishara watumie Brela katika kurasimisha biashara zao ili wapate faida za kutambulika wanapofaya biashara na uzuri utaratibu wa urasimishaji umerahisishwa kwa njia ya mtandao,”amesema

Ofisa Mtendaji  Mkuu wa Brela,Godfrey Nyaisa amesema hadi sasa ndani ya mwaka huu wa fedha kampuni zilizosajiliwa na taasisi ni 7148  na malengo yao ni kusajili makampuni 9528 ambapo hadi sasa usajili umefikia asilimia 75.

Amesema kwa sasa usajili wa kampuni unakamilika ndani ya siku moja,changamoto hutokea endapo anayesajili amewasilisha nyaraka zenye kutiliwa mashaka na wataalam kutoka kwao au kuwasilisha nyaraka zisizokamilika.