November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mkenda: Elimu ni mtaji wa Taifa kusonga mbele

Na Mwandishi wetu, Timesmajira OnlineĀ 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema elimu ndio mtaji na kwamba itabadilisha taifa liweze kusonga mbele.

Waziri Mkenda amesema hayo Mkoani Tanga alipokuwa akizindua Kampeni ya Niache Nisome Pangani Inanitegemea iliyobuniwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mhe. Zainabu Abdallah.

Amesema nchi inahitaji wataalam wazuri katika fani mbalimbali akitolea mfano madaktari, walimu na wahandisi ili iweze kusonga mbele hivyo ni vizuri kuwaacha watoto wasome ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Elimu ni ufunguo wa maisha ukimnyima mtoto elimu unamnyima maisha, mafanikio ya watu waliosoma ni chachu katika kuleta mabadiliko,” amesema Prof. Mkenda

Akizungumzia kampeni ya Niache Nisome Pangani Inanitegemea inayofanyika katika Halmashauri ya Pangani Mkoani Tanga   Waziri Mkenda amempongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Zainabu Abdallah pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Jumaa Aweso na kusema kuwa kuna la kujifunza kutoka katika halmashauri hiyo ili kuleta mageuzi ya elimu na amehimiza watu kujifunza kwenye mambo mazuri kama hayo.

Kufuatia ombi la Mhe. Aweso kuhusu VETA ya wilaya hiyo  kuanza kutoa mafunzo  Prof. Mkenda amemuahidi kuhakikisha VETA zote za Wilaya za mkoa wa Tanga zinaanza  kutoa mafunzo mwezi Septemba mwaka huu.

Pia amesema kuwa kwa maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuweka Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 ambayo haina na Vyuo hivyo, Tanga inakwenda kupata Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Sekiboko amemuomba Waziri Mkenda  kuupa Mkoa wa Tanga kipaumbele kwa fursa za elimu hasa wilaya ya Pangani kwa kuwa ni moja ya wilaya ambayo wanafunzi wanatembelea umbali mrefu kufuata shule.

“Mhe. Waziri wanafunzi wanatembea umbali mrefu kuifuta shule katika wilaya hii, niliamua kutoa fedha zangu kuwaweka hostel kutokana na changamoto hiyo ili  kuwaepusha na vishawishi njiani naomba fursa yoyote ikitokea ilete Pangani,”amesema  Mhe. Sekiboko

Nae Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Jumaa Aweso amemshuru Waziri Mkenda  kwa kuwajengea VETA ya wilaya na kumuomba amfikisie salamu hizo kwa Mhe. Rais huku akimuomba kuifanya shule ya Funguni iliyopo wilayani humo kuwa na kidato cha tano na sita. 

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Zainabu Abdallah amesema katika Halmashauri hiyo wameamua kuifanya elimu kipaumbeleĀ  kutokana na wilaya hiyo kuwa nyuma kielimu na kwamba kupitia Kampeni waliyoianzisha ya Niache Nisome Pangani Inanitegemea halmashauriĀ  hiyoĀ  itakuwa na mageuzi makubwa kwenye elimu.