Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Elimu,Prof.Adolf Mkenda ametoa maelekezo kwa walimu wote nchini kutowarudisha wanafunzi nyumbani wazazi wao wanaposhindwa kutoa michango mbalimbali waliyokubaliana.
Prof.Mkenda ametoa maelekezo hayo jijini hapa leo Aprili 5,2024 wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa pamoja wa tathmini ya Sekta ya elimu kwa mwaka 2023/2024 uliohusisha wadau mbalimbali wa elimu kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo kwenye Sekta hiyo na kuleta mageuzi katika elimu.
Prof.Mkenda amesema kuwa licha ya makubaliano ya wazazi na walimu kutoa michango ikiwemo chakula lakini si vyema kumrudisha mwanafunzi nyumbani au kumkamata mzazi kwa kushindwa kilipia michango hiyo.
Hivyo amewataka walimu wawaache wanafunzi waendelee na masomo huku akisisitiza wazazi kuchanga michango waliyokubaliana hasa chakula kwani Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema elimu bila malipo lakini watoto wakipata chakula itawasaidia kuelewa wanachojifunza.
Ameeleza kuwa hakuna utaratibu wa kiserikali wa kumrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kukosa michango kwa kuwa dhana ya elimu bila ada inaelekeza mtoto asinyimwe kwenda shule kwa kukosa michango na kufafanua kuwa hakuna adhabu yoyote itakayofanya mtoto akose masomo.
Waziri Mkenda amesema licha ya changamoto zilizopo kwenye Sekta hiyo,Walimu wanapaswa kuheshimiwa ili kuwafanya wanafunzi kuwa bora huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuleta mageuzi kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu.
Kwa upande wake Kamishina wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa ametaja mambo muhimu yaliyojadiliwa katika kikao chicho kilichowachukua muda wa siku tatu ambapo ameeleza kuwa wamejadili na kuazimia kwenda kuyafanyia kazi maeneo 10 ambayo yataleta ufanisi katika wa kisekta.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni kuboresha vikao na mikutano ya pamoja ya tathimini katika sekta ya elimu ili kuleta matokeo chanya na kuboresha mpango wa chakula na lishe mashuleni ambapo wameazimia ikiwezekana sheria itungwe ya kuwataka wazazi wachangie masuala mazima ya elimu pale inapobidi kwani bila afya akili hakuna.
Maadhimio mengine ni kwenye eneo la mitaala ambapo wametaka kupelekwe Sera za mitaala ili kulahisisha wadau walimu katika utendaji kazi
Jambo jingine amesema waneona elimu ya juu ihakisi mabadiliko yote yalifanyika kuanzia elimu ya ngazi ya chini, bila kusahau kuimalisha ushirikiano kati ya wizara na wadau Mbalimbali wanaotoa elimu hapa nchini na nje ya nchi
Aidha amesema eneo lingine ni kuhakikisha wanajikita katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi bila kusahau hisabati pia na kutafuta mbinu na mikakati ili kupata rasilimali kuendesha elimu
Hata hivyo amesema eneo lingine ni kwenye elimu ya watu wazima imesahaulika mfumo wake, lakini pia uchangishwaji wa elimu kwa jamii na sio lazima iwe ni fedha pekee na serikali na wadau kupeana mafunzo Mbalimbali juu ya elimu.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo