October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mbamba: Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri ya kupeleka bidhaa Misri

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa, Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri ya kupeleka bidhaa za chakula, umeme na biashara zingine nchini Misri.

Hayo ameyasema leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Profesa Ulingeta Mbamba kwenye kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Misri katika maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

“Kama Tanzania tunavitu vingi vya kujifunza na kuwapelekea wenzetu katika nchi ya misri, tunazungumza masuala ya chakula, umeme n.k, ni nchi iliyo katika nafasi nzuri kwa Tanzania kama tutaitumia vizuri na hata watu wa misri watakuwa na nafasi nzuri ya kutumia katika nchi yetu ya Tanzania”

Amesema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inatoa bidhaa za dola milioni moja, ambapo Tanzania inachukua bidhaa za dola milioni 60 kutoka Misri.

Mbali na hayo amesema kupitia siku hiyo imetoa fursa kwa wafanyabiashara kuonesha nini ambacho hufanya katika nchi hizo mbili.

“Siku ya Egypt tumeweza kusikia nini kilichopo katika nchi ya misri na nini tunaweza kufanya katika nchi ya Tanzania kwaajili ya nchi ya Misri”

Alifafanua kuwa mikutano ya kibiashara kati ya nchi hizo imefanyika na inaendelea kufanyika huku akitarajia mazuri zaidi katika biashara kati ya nchi hizo.

Kwa upande wake Meneja Uenezi na masoko, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar(ZIPA), Khamis Dunia amesema wameshiriki katika maonesho hayo ili kutafuta wawekezaji zaidi.

“Mwamko ni mzuri taasisi 36 kutoka Misri zimeshiriki katika maonesho ya Sabasaba na sekta mbalimbali zimeshiriki ikiwemo ujenzi, sekta ya uhandisi na zingine zinazohusiana na uchumi wa bluu,”amesema.

Amesema Zanzibar inatangaza fursa zilizopo katika uchumi wa buluu (bahari na pembezoni mwa bahari) ambazo ni utalii, uvuvi, ukulima wa baharini, usafiri wa bahari.

Amesema Zanzibar wamegundua mafuta na gesi ambayo wanatafuta wawekezaji, sekta ya ujenzi wa nyumba za biashara na makazi.

“Tupo kutafuta wawekezaji kutoka Misri na ili kuwekeza Zanzibar,”alisema.

Aidha Balozi wa Misri nchini Tanzania,  Shariff Ismail amepongeza maonesho hayo ambayo ameona mabadiliko ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana.

Ameongeza kuwa , mwaka huu katika maonesho hayo yameshiriki makampuni 26.

“Hii siku ni muhimu sana Misri na Tanzania tunaadhimisha miaka 60 ya uhusiano , katika historia tunauhisiano imara …kama balozi tunatafuta njia za kuimarisha uhusiano wetu kwasababu watu wetu na historia yetu inastahili kushirikiana,”alisema.

Alisema kupitia mkutano huo, matunda yataonekana baina ya nchi hizo mbili kupitia ushirikiano katika biashara na uwekezaji na kukuza uchumi.