January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Lipumba akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Musoma hawapo pichani

Prof: Lipumba aahidi kuongezaa ajira,kuanzisha viwanda

Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online,Mara

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) Prof.Ibrahimu Lipumba, amewaomba Watanzania wampe ridhaa kwa kumchagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kusudi aweze kuongeza ajira za kada mbalimbali kwa kuajiri Wafanyakazi sambamba na kuanzisha Viwanda vingi ambavyo vitaongeza thamani ya mazao ikiwemo Viwanda vya nguo na Viwanda vya kilimo.

Prof. Lipumba akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Musoma hawapo pichani

Ameyasema hayo wakati akiomba kura na kunadi sera za chama hicho kwa Wananchi wa Manispaa ya Musoma, katika uwanja wa Shule ya Msingi Mukendi hii leo ambapo pamoja na mambo mengine amesema zao la pamba na Mhogo linamchango mkubwa wa Maendeleo kwa Wakazi wa Mkoa wa Mara kutokana na ardhi nzuri hivyo akichaguliwa ataanzisha Viwanda hivyo Mkoani Mara.

“Madaktari hawaja ajiriwa kwa wingi licha ya kuhitimu masomo yao, na pia Walimu, na Wahitimu wa fani nyingine nyingi, Kama hakuna ongezeko la wafanyakazi wenye mishahara kila mwezi usitegemee mzunguko mkubwa wa fedha Nchini, pia makandarasi wengi hawalipwi kwa wakati, Benki kuu imeshindwa kuongeza ugavi wa fedha nchini naomba mnichague Oktoba 28 mwaka huu kusudi uchumi wa Nchi nikausukume ukue kila mwaka asilimia kwa asilimia 10.” amesema Prof. Lipumba.

Ameongeza kuwa,iwapo atachaguliwa itaongeza idadi kubwa ya viwanda vya pamba katika Mikoa ya kanda ya ziwa na nchini kwa ujumla, vitakavyozalisha Nguo kwa wingi na kuwezesha wakulima wa zao hilo kulipwa bei nzuri ambayo wakulima itawanufaisha na kuwafanya waendelee kujikita katika kilimo hicho kwa ufanisi tofauti na ilivyo sasa.

“Mapinduzi ya Viwanda huanza na Viwanda vya Nguo ambavyo ni vyepesi kabisa kuanzisha, lakini cha kushangaza sekta ya Viwanda nchini inasuasua kwa hiyo usitegemee itaongeza ajira bila Viwanda kuwepo, mfano kiwanda Cha Musoma Cha Maziwa kimekufa na kiwanda Cha Samaki kilichokuwepo,, usitege uchumi kukua, hatuwezi kuleta mapinduzi ya viwanda bila kuwa na mapinduzi ya kilimo chenye tija” amesema Lipumba.

Sehemu ya Wananchi wa Musoma wakifuatilia hotuba ya mgombea urais wa Tanzania kupitia CUF

Ameongeza kuwa, kuongeza tija kwenye kilimo ndiko kunawezesha watu wengine waajiriwe katika sekta nyingine, na hivyo amesema endapo atashinda atahakikisha kwamba Serikali yake inaweka mkazo thabiti katika kilimo kwa kuongeza bajeti ya kutosha katika kilimo na utafiti wa mbegu bora, pembejeo ili kuwezesha wakulima kulima mazao yanayokubalika katika eneo linaloruhusu zao hilo.

Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba amesema kuwa akichaguliwa serikali yake itaimarisha sekta ya Afya kwa kudhibiti vifo vya Kinamama wanaojifungua nchini kwa kuhakikisha wanajifungua salama kwa kuongeza ubora wa lishe ili Mtoto mchanga azaliwe katika hali njema katika kujenga Taifa lenye afya katika kufanya shughuli za maendeleo.

“Tunahitaji pia kuwa na Katiba mpya, zoezi la kupata Katiba mpya lazima liweze kufanyika endapo mtanichagua kusudi nifanye hivyo, pia nitaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa vyama vyote ambavyo havina wawakilishi Bungeni lazima vipate wawakilishi ili tuwe na Katiba itakayoweza kushughulikia suala la rushwa na ufisadi, na kutetea haki kwa Wananchi huu ni wakati muhimu Sana kuleta mabadiliko ya dhati,” amesema Prof.Lipumba.

Kwa upande wake mgombea ubunge kupitia CUF,Jimbo la Musoma Mjini Maimuna Matollah amesema akichaguliwa atashughulikia matatizo ya Wakazi wa Musoma Mjini kwa kuwasemea Bungeni kwa ufanisi.

Prof.Lipumba alifanya mikutano mitatu akiwa mkoani Mara katika Wilaya ya Bunda, Musoma Vijini, na Manispaa ya Musoma.