December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kitila awafidia bodaboda waliounguliwa na pikipiki wakati wa ajali

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amekabidhi pikipiki mbili kwa vijana wa Bodaboda ambao pikipiki zao ziliteketea kwa moto wakati wa ajali ya roli la mafuta mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Ubungo Kibo Dar es Salaam.

Akikabidhi pikipiki hizo Prof. Kitila amesema aliguswa na kupotea kwa ajira za vijana hao alipotembelea eneo la ajali na kuahidi kuwasaidia na ametimiza ahadi hiyo.

Amesema pikipiki hizo ni kwaajili ya waendesha pikipiki ambao ajira zao zimepotea na siyo wamiliki huku akiahidi kuweka Mwanasheria atakayewasaidia wafanyabiasha ambao bidhaa zao ziliteketea siku hiyo ya ajali.

“Ili mpate haki ya malipo yenu ni lazima muwe na Mwanasheria maana hili ni Jambo la kisheria, hivyo Mwanasheria atakuja mtakaa naye na kuanza mchakato wa kudai Bima” amesema Prof. Kitila Mkumbo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kibo Sophia Fitina amemshukuru Mbunge wao ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kuwakimbilia kila wakati na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.

“Ijumaa ya leo imekuwa ni ya pekee kwetu na ya faraja, maana siku moto ulipotokea Wananchi walikimbia wakaacha nyumba wazi, maduka wazi na hakuna aliyekumbuka kufunga mlango lakini hakuna mtu aliyeibiwa hata kijiko hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu” Sophia Fitina Mwenyekiti Mtaa wa Kibo

Kwa upande wao Vijana waliokabidhiwa pikipiki hizo ambao ni Mkwayu Said na Daru Kibwana Omari wamemshukuru Mbunge wao na kueleza kuwa siku walipofikwa na madhira ya kuunguliwa pikipiki zao walipoteza mwelekeo lakini sasa wamepata tumaini jipya.

“Tunaishi kwenye Jimbo la Ubungo miaka mingi lakini hatujawahi kuona Mbunge wa eneo hili akitimiza ahadi zake kwa wakati kama alivyofa ya Mbunge wetu Prof. Kitila, anapaswa kupongezwa” Vijana waliokabidhiwa pikipiki