January 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kikula aitaka menejimenti ya tume ya madini kuchapa kazi kwa bidii

Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online

MWENYEKITI wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula ameitaka Menejimenti ya Tume ya Madini kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli linalotolewa na Serikali kila mwaka hivyo mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kuzidi kuongezeka.

Profesa Kikula ametoa agizo hilo leo Mei 11, 2022 kwenye kikao cha Kumi na Nne cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Amesema kuwa, menejimenti ya Tume ya Madini kuendelea kuongeza bidii kwenye utendaji kazi kutapelekea mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini na kujenga taswira chanya kwa Taasisi.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuendelea kuwahudumia wananchi wa ubunifu na uzalendo wa hali ya juu.

Wakati huohuo akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Tume ya Madini katika kikao hicho Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2022 viongozi wa Tume walifanya ziara za kikazi katika maeneo mbalimbali yenye shughuli za madini nchini lengo likiwa ni kutatua changamoto za wachimbaji na wafanyabiashara ya madini.

“Kupitia ziara hizo, viongozi walikagua shughuli mbalimbali za madini ikiwa ni pamoja na utendaji kazi wa ofisi, masoko ya madini yaliyo kwenye mikoa na hatua iliyofikiwa katika lengo la ukusanyaji wa maduhuli,” amesema Mhandisi Samamba.

Aidha, ametaja shughuli zilizotekelezwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2022 ni pamoja na uchambuzi wa maombi ya leseni za uchimbaji mkubwa wa madini, usimamizi wa masuala ya kisheria, ukaguzi wa mabwawa ya kuhifadhia topesumu, utunzaji na matumizi ya baruti na uchambuzi wa Mipango ya ufungaji Migodi.

Wakati huohuo akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye Sekta ya Madini, Kamishna wa Tume ya Madini Janet Lekashingo amesema kuwa Tume ya Madini ina jukumu la kusimamia ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ili kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zilizopo katika Sekta ya Madini pamoja na kufungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi.

Amesema kuwa, Tume ya Madini kupitia Kamati hiyo imekuwa ikichambua mipango inayowasilishwa na kampuni zote zinazojishughulisha na uchimbaji wa madini pamoja na watoa huduma katika Sekta ya Madini kama takwa la Sheria ya Madini Sura 123 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka, 2018.

“Tume ya Madini kupitia kamati hii inaendelea kutekeleza kwa kuhakikisha kampuni zinazowekeza katika Sekta ya Madini zinatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini, kutoa kipaumbele cha ajira na mafunzo kwa Watanzania, pamoja na kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na Watanzania au Kampuni za Watanzania,” amesema.

Kikao cha Kumi na Nne cha Tume ya Madini kimehudhuriwa na Makamishna wa Tume ya Madini, Menejimenti na Wataalamu kutoka Tume ya Madini.