March 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Kabudi atoa maagizo Saba Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari

Na Penina Malundo,Timesmajira

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof.Palamagamba Kabudi amezindua rasmi Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (Journalists Accreditation Board-JAB) huku akitoa maagizo saba kwa bodi hiyo.

Miongoni mwa maagizo hayo aliyoyatoa ni pamoja na kuhakikisha kuwa, waandishi wa habari wote nchini wanazingatia sheria, kanuni, viwango vya juu vya weledi, maadili, uwajibikaji, na miongozo inayosimamia taaluma ya uandishi wa habari.

Akitoa maagizo hayo  jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi ya bodi hiyo,Prof.Kabudi   amesema, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari itasaidia kudhibiti uandishi usio wa kimaadili na kuongeza heshima ya taaluma hiyo, hivyo inatakiwa kuanza kwa kuwalea na kuwapa miongozo mbalimbali kuhusu taaluma yao.       

                               

                                                                                                       

Profesa Kabudi ameitaka pia Bodi hiyo kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanazingatia maadili ya taaluma kwa kutoa miongozo ya mafunzo ya mara kwa mara, na kuwa na utaratibu wa kushughulikia malalamiko na ukiukwaji wamaadili kwa haki na uwazi.                                                                                                         Akitoa agizo la pili kwa Bodi ni kuandaa na kusimamia utaratibu wa usajili wa waandishi wa habari kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, huku akisisitiza kuwa mfumo huo unatakiwa kua shirikishi na wenye kuendana na maendeleo ya teknolojia na mazingira ya sasa ya sekta ya habari.                                                                                 

Ameitaka JAB kuhakikisha inashirikiana na vyombo vya habari, vyuo vya mafunzo ya uandishi wa habari, na wadau wengine ili kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mafunzo ya mara kwa mara na kuwa na ujuzi wa kisasa.       

                                                                        Prof.Kabudi ameiagiza Bodi kuandaa programu za uelimishaji ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa taaluma ya uandishi kusimamiwa ipasavyo.                                                                                               

Amesisitiza kuwa ni muhimu Bodi pia ikasaidia kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanatumia teknolojia kwa manufaa ya taaluma yao bila kuvunja maadili, katika ulimwengu wa sasa wa kidijitali, ikiwemo kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika utoaji wa habari.                                     

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi Bodi inapaswa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa usalama bila vitisho, unyanyasaji, au vikwazo visivyo vya lazima, kwani Usalama wa wanahabari ni msingi wa uhuru wa vyombo vya habari.                

Akitangaza kuzinduliwa rasmi kwa Bodi hiyo, Prof.Kabudi amesema, Serikali inatambua umuhimu wake, katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na kuahidi kuwa itaendelea kushirikiana nayo ili kuhakikisha taaluma ya habari inaimarika kwa manufaa ya taifa. 

Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 ya Sheria za Tanzania, ipo chini ya Mwenyekiti Mzee Tido Mhando.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Gerson Msigwa, amesema Bodi ya Ithibati chini ya Wizara hiyo, itakuwa na jukumu la kusimamia maadili ya taaluma na kusaidia kukuza mazingira bora ya utendaji kazi katika Sekta ya Habari hapa nchini.

Amesema kuwa Bodi hiyo itawajibika kuhimiza waandishi wa Habari kuandika kwa weledi, na kuzingatia ukweli, haki na maslahi ya umma. 

Amebainisha kuwa Bodi ya Ithibati yenye wajumbe 7 akiwemo Mwenyekiti wake Ndugu Tido Mhando, itashirikiana na Taasisis za mafunzo na wadau mbalimbali wa tasnia ya Habari kuhakikisha waandishi wa Habari wanapata elimu bora na mafunzo yanayokidhi viwango vya kitaaluma. 

Akitoa shukurani zake Mhando amemuhakikishia Waziri Kabudi kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wamepokea maelekezo aliyowapa na kwamba watayatekeleza kwa moyo wa uzalendo, uadilifu na ufanisi wa hali ya juu kwa ushirikiano na wadau wa sekta ya Habari.

Amesema kwa kuonyesha utayari wa kufanya kazi, vikao vya Bodi ya ithibati vitaanza Jumanne Machi 4;2025, kwa lengo la kupanga mikakati mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo yaliyoainishwa kwa mujibu wa sheria.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula, amewataka waandishi wa Habari kuilinda taaluma ya uandishi wa Habari kwa kuwa hakuna atakayeilinda zaidi ya wao wenyewe.