November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA:Rushwa inatuletea wazabuni wasiyo na sifa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Udhibiti ununuzi wa umma(PPRA)imetaja changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo kwa upande wa Taasisi Nunuzi na wazabuni ikiwemo vitendo vya Rushwa ambavyo vinapelekea kupata wazabuni wasiyo na sifa.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Julai 17 ,2023 na Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA,Eliakim Maswi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa utekelezaji wa mamlaka hiyo kwa mwaka 2023/24 ambapo amesema Ununuzi wa umma unakabiliwa na hatari kubwa ya rushwa, Watendaji na maafisa Serikalini wamekuwa wakilalamikiwa na kuhisiwa kuwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa Mikataba au kuwapa faida zisizo halali Wazabuni wasiyo na sifa.

“Hii inapunguza ushindani na kusababisha upotevu wa fedha za umma,”amesema Maswi.

Maswi ametaja changamoto nyingine kuwa ni
Uwazi usiyoridhisha kwenye mchakato wa zabuni
ambapo amesema kosefu wa uwazi katika mchakato wa ununuzi wa umma kunasababisha changamoto za upatikanaji wa taarifa za zabuni, thamani ya mkataba na kusababisha ukosefu wa uaminifu na Imani kwa Taasisi za Umma pia hata wananchi wanakosa Imani kwa Serikali kutokana na Matumizi yasiyoeleweka.

Aidha amesema changamoto nyingine ni Mchakato wa zabuni kuchukua muda mrefu,Kutozingatia taratibu za Ununuzi wa umma,Ukiukwaji wa taratibu na miongozo ya ununuzi wa umma hivyo kupelekea upendeleo (mikataba kutolewa kwa makampuni yasiyostahili kwa kutozingatia vigezo vya sheria), kutokuwepo kwa ushindani na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Kwa Wazabuni,Wazabuni kuwasilisha bidhaa au huduma zisizoridhisha au zilizo chini ya viwango.

“Chamagamoto nyingine ni bei za bidhaa, huduma na kandarasi kuwa kubwa kuliko uhalisia wa bei za soko,Wazabuni wasiyokuwa na uwezo au vigezo kuomba zabuni za Serikali suala hili hupelekea mchakato wa ununuzi kuchukua muda mrefu na Baadhi ya Wazabuni wasiyo na uwezo kushawishi na kutoa rushwa,”amesema Maswi.

Pamoja na hayo Maswi amesema kuwa
Serikali imeendelea kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mifumo ya kielektroniki ili kuleta tija na ufanisi unaostahili katika utekelezaji wa Bajeti husika.

“Kwa takribani miaka minne, Serikali imekuwa ikitumia mfumo wa TANePS ambao umegubikwa na changamoto mbalimbali na Baadhi ya changamoto hizo ni kutokuwa rafiki kwa watumiaji, kuwa na hitilafu za kiufundi za mara kwa mara; na mfumo kuwa na mianya ya kuwezesha Taasisi kutotumia mfumo hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wazabuni na Taasisi Nunuzi.

“Wazabuni kulalamika kwa kukosa uwazi, ushindani wa haki lakini kibaya zaidi bidhaa, kazi na huduma kukosa thamani halisi ya fedha na kuleta malalamiko na Hoja nyingi za ukaguzi.

“Hivyo kwa kuzingatia changamoto zilizopo, Serikali ilifanya maamuzi ya kujenga mfumo mpya. Mfumo mpya unajulikana kwa jina la “National e-Procurement System of Tanzania (NeST),”ameeleza Maswi.