November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA Tanzania ,Bangladesh wabadilishana uzoefu matumizi ya mifumo na TEHAMA

Na Mwandishi wetu

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Eliakim Maswi ameongoza ujumbe wa Mamlaka na Taasisi nyingine za Serikali kwenye ziara ya kikazi ya siku tano nchini Bangladesh.

Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu kwenye matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma.

Ujumbe kutoka Tanzania umejumuisha watumishi kutoka PPRA, Wizara ya Fedha na Bohari ya Dawa (MSD).

Akizungumza Jumatatu hii katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ya Bangladesh (BPPA) jijini Dhaka, Bw. Maswi amesema kuwa wamefanya ziara hiyo wakati huu ambapo Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) unaonesha mafanikio makubwa nchini hali inayopelekea Mamlaka kuendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu zaidi kuhusu matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwenye ununuzi wa umma hasa kwa nchi ambazo tayari wana mifumo ya ununuzi ya kielektroniki.

Ameongeza kuwa kwakuwa Bangladesh ni moja kati ya nchi zilizofanikiwa zaidi kwenye matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika ununuzi wa umma, watajadili jinsi walivyoweza kutatua changamoto mbalimbali na kuimarisha mifumo yao.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BPPA, Mohammed Shoheler Rahman akiwa na viongozi wengine wa Mamlaka hiyo walifanya wasilisho kuhusu Mfumo wanaoutumia kusimamia ununuzi wa umma nchini Bangladesh. Bw. Rahman alisema kwa upande wa Bangladesh mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (e-GP) ulianzishwa rasmi mwaka 2011 na kufanyiwa mabadiliko makubwa September 2023.

Mfumo wa NeST ulianza kutumika rasmi Julai 2023, ambapo Serikali ya Tanzania ilielekeza kuwa michakato yote ya ununuzi ifanyike kupitia mfumo huo ikiwa hadi sasa zaidi ya wazabuni 17,000 wamejisajili, bajeti ya zaidi ya Sh. 26 Trilioni zimewekwa kwenye mfumo na mikataba ya zaidi ya Sh. 2.8 trilioni imetolewa kwa wazabuni.