March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPPC yasisitiza umuhimu wa uwekezaji kupitia ubia katika sekta ya Umma na Sekta binafsi

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online

UBIA kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (PPP) unaendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha huduma kwa umma kupitia ushirikiano wenye tija, ubunifu na ufanisi mkubwa.

 Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila , alipokuwa akizungumza kuhusu nafasi ya PPPC katika kuhakikisha utekelezaji madhubuti wa miradi ya PPP nchini.

Kwa mujibu wa Kafulila, mfumo wa PPP nchini Tanzania umejengwa juu ya misingi imara ya kisheria na kitaasisi inayolenga kuvutia wawekezaji binafsi kushiriki katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa huduma bora kwa umma kwa gharama nafuu.

Mfumo wa kisheria wa PPP

Amesema,kwa sasa, utekelezaji wa miradi ya PPP unasimamiwa na jumla ya sheria tisa, ikiwemo,Sera ya Taifa ya PPP ya mwaka 2009,Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya PPP 2021/22–2025/26,Sheria ya PPP (Sura ya 103) iliyofanyiwa marekebisho,Kanuni za PPP za mwaka 2020 (ziliyorekebishwa mwaka 2023),Sheria ya Madeni (Sura ya 134),Sheria ya Bajeti (Sura ya 439),Sheria ya Uwekezaji (Sura ya 38),Sheria ya Manunuzi ya Umma (Sura ya 410), naSheria ya Kampuni (Sura ya 212).

Amesema,Sheria hizi zinasimamia hatua zote muhimu za mzunguko wa maisha ya mradi, kuanzia uibukaji wake, upembuzi yakinifu, uteuzi wa mbia, ujenzi, uendeshaji na hatimaye kurejeshwa kwa serikali.

Lengo la  PPP: Huduma bora kwa gharama nafuu

Amesema,”Ubia huu ni mkataba wa muda mrefu unaoingiwa kati ya serikali na mwekezaji binafsi ambapo kwa kutumia ubunifu, utaalam na teknolojia kutoka sekta binafsi, miundombinu inaboreshwa au kujengwa upya kwa lengo la kutoa huduma bora na nafuu kwa umma,”

Aliongeza kuwa, kwa kuwa sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kifedha, kitaalam na kiteknolojia, ubia huu huipa serikali nafasi ya kuokoa gharama za uwekezaji mkubwa wa awali huku ikihakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.

Upatikanaji wa wawekezaji wa PPP

Kwa mujibu wa  Kafulila, mwekezaji wa PPP hupatikana kwa njia nne ikiwemo njia ya ushindani wazi,njia ya kutokushindanishwa  hasa kwa miradi inayoibuliwa na sekta binafsi inayokidhi vigezo vilivyoainishwa chini ya kifungu cha 15(2) cha Sheria ya PPP,mazungumzo ya moja kwa moja  kwa miradi ya serikali iliyopitia mchakato maalum, na utaratibu maalum  ambapo mkataba huwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maoni, kisha kupelekwa Baraza la Mawaziri kwa idhini.

Vipimo vya ubora wa Mradi

Amebainisha kuwa miradi ya PPP hupimwa ubora wake kwa vigezo vitatu kuu ikiwemo Je, sekta binafsi imebeba sehemu kubwa ya hatari za mradi (mianya hasi)?Je, huduma zinazotolewa ni nafuu kwa wananchi?na Je, ubia huo unaleta manufaa halisi kwa serikali na umma?

“Kwa kuzingatia haya, tunaweza kuhakikisha kwamba PPP sio tu mkataba wa kibiashara bali ni mkataba wa maendeleo na uwajibikaji kwa wananchi,” alisisitiza Kafulila.

Aidha kwa kuimarisha mfumo wa kisheria na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu mchakato wa PPP, Tanzania imo katika njia sahihi ya kuvutia wawekezaji zaidi na kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya miundombinu, huduma za kijamii na uchumi kwa ujumla. PPPC, kwa usimamizi wake makini, inahakikisha kuwa ubia huu unakuwa wa manufaa ya pamoja  kwa serikali, sekta binafsi na wananchi.