January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi yatoa mafunzo kwa mafundi magari Stendi ya Magufuli

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira. Online

JESHI la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, limetoa mafunzo kwa mafundi magari waliyokuwa ndani ya Kituo cha Mabasi cha Magufuli Mbezi Luis, Dar es Salaam kwa lengo la kuwafundisha jinsi ya kutambua vifaa ambavyo vipo kwenye magari hayo.

Mafunzo hayo yametolewa na Mkuu wa Usalama Barabarani, ASP Ibrahim Samwix kwa lengo la mafundi hao kutambua mfumo wa injini ya gari unavyofanya kazi ili kuwaraisishia namna ya utengenezaji wa magari.

Pia amewafundisha kuhusu kifaa cha aina ya turbo kinavyofanya kazi na namna ya kukitambua kama kikiwa kibovu kwa sababu mafundi wengi wamekuwa wakifanya masuala ya ufundi kwa mazoea.

Ametoa pia mafunzo katika kifaa cha mfumo wa rejeta namna kinavyofanya kazi kwa sababu mafundi wengi na madereva, wamekuwa wakishindwa kutunza mabasi wanayopewa kutokana na upungufu mdogo mdogo.

Kabla ya mafunzo hayo, Mkuu huyo ameanza na madereva kwa kuwaelimisha jinsi ya kufuata sheria za barabarani na kuendesha gari kwa mwendo ambao unatakiwa, ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya wananchi.

Kwa wa upande wa madereva hao ambao walikuwa zaidi ya 40, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa mafunzo hayo kwa sababu yanawakumbusha kufuata sheria za barabarani, kutokana na kwamba wengi wanafanya kazi hiyo kwa mazoea.

Pia wamesema ni mara yao ya kwanza kupatiwa mafunzo kwa hiyo wao wameona ni bahati kubwa kwa sababu wamejifunza mambo mengi kwa wakati mmoja kwa sababu wakati mwingine, wanahisi kuwa mesahaulika.

Waneomba elimu hiyo na mafunzo hayo, yawe endelevu kwa manufaa yao na kwa manufaa ya watumiaji wa barabara, wao wapo tayari muda wowote na pia wataendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Naye Athuman Omary ambaye ni mkazi wa Tabata, Dar es Salaam ametoa shukrani kwa jeshi hilo kwa elimu ambayo walikuwa wanaitoa kwa madereva na wamiliki wa mabasi kwa sababu inaonesha ni jinsi gani wanajali maisha ya abiria.

Pia mkazi wa Ubungo, Mwajuma Juma amewata madereva hao kutumia mafunzo waliyoyapa kwa kupunguza ajali za barabarani kwa sababu kuna baadhi ya madereva hawafuati sheria hizo kwa makusudi.

Wamiliki wa mabasi, wamelipongeza jehi hilo kwa mafunzo ambayo wamepewa madereva wao pamoja na mafundi wa mabasi, ambapo wamesema hiyo itaondoa ajali za barabarani, itasaidia ulinzi wa magari yao na pia ushirikiano baina ya askari na wao utakuwa wa manufaa.