Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limeungana na watoto wanaoishi katika kituo cha kulelea Yatima kijulikanacho kwa jina la Maasai Girls Rescue Center kilichopo wilaya ya Karatu kwa lengo la kuwaleta karibu watoto na jeshi hilo ili kupata taarifa za matukio ya ukatili.
Tukio hilo limefanyika leo Januari 28 mwaka huu ambapo Mkuu wa Polisi wilaya ya Karatu Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Radegunda Marandu amesema jeshi hilo limetoa misaada mbalimbali kwa yatima hao ikiwa ni mkakati wa kuifanya jamii kuwa karibu nao ili wapate taarifa za uhalifu hususani za ukatili wa kijinsia na watoto.
SSP Marandu amebainisha kuwa pamoja na kuwa jeshi hilo linahusika na ulinzi wa raia na mali zao pia wanalojukumu la kushirikiana na wananchi katika matukio ya kijamii ikiwemo la kuonyesha upendo kwa yatima ambapo watakua huru kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo za ukatili.
Sambamba na hilo pia ametoa onyo kwa watu wachache ambao wanatabia ya kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili kuacha mara moja kwani jeshi hilo lipo makini na litachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
Naye Bwana Elisante Loi, meneja wa kituo hicho amesema msadaa uliotolewa utawafanya watoto hao kujua kuwa Polisi ni sehemu ya jamii hivyo watakua huru kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa jeshi hilo bila kuogopa.
Sambamba na hilo awewataka wazazi kuacha tabia ya ukatili kwa watoto kwani unasabisha madhara makubwa ikiwemo tatizo la kisaikolojia hata kupelekea umauti.
Momoi Daniel kwa niaba ya watoto wenzake pamoja na kushukuru msaada uliotolewa pia amewataka watoto wenzake ikiwa watakutana na changamoto au tatizo hususani za ukatili wasikae kimya au kuogopa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best