December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi watatu kortini kwa tuhuma ya rushwa Tunduma

Na MWandish Wetu,Timesmajiraonline,Momba.

ASKARI Polisi watatu wa kituo cha Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoani Songwe, wamefikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa kiasi cha shilingi milioni 55.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe imewafikisha askari hao, leo Juni 4, 2024 katika mahakama ya Wilaya ya Momba iliyopo eneo la Chapwa, Mjini Tunduma.

Askari hao ambao tayari wameshafukuzwa kazi na jeshi la polisi kabla ya kukamatwa na Takukuru kisha kufikishwa mahakamani hapo ni Koplo Enock Marando (43), Koplo Samson Kalebe (38), pamoja na Konstebo wa polisi Zawad Malakasuka (39).

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba, Timoth Lyon, mwendesha mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Simona Mapunda, alidai kuwa washitakiwa walitenda makosa hayo, Machi 7 mwaka huu katika mpaka wa tunduma.

Mapunda alidai kuwa, siku ya tukio washitakiwa wakiwa ni waajiriwa wa jeshi la polisi waliomba rushwa ya shilingi milioni 55 ambapo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) na (2) cha makosa ya rushwa kutoka kwa mfanyabiashara Halima Abdallah ambaye ni mfanyabiashara ili wamsaidie baada ya kumkamata na shehena ya vipodozi vilivyopigwa marufuku.

Hakimu Lyon, baada ya kusikiliza maelelezo ya kesi hiyo ya rushwa namba 15094 ya mwaka 2024 na watuhumiwa wote kukana kutenda makosa hayo aliahirisha shauri hilo hadi Juni 18 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itarudi mahakamni hapo kwa ajili ya kuanza kusikiliza hoja za awali.

Hata hivyo, Washitakiwa hao walikosa dhamana na kurejeshwa mahabusu baada ya wadhamini wao kushindwa kukikidhi masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama hiyo.

Masharti hayo, yalitaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya shilling million 22.5 kila mmoja wao, pamoja na washitakiwa hao kutakiwa kuwasilisha dhamana ya maandishi ya kiasi cha shilling million 19 Kila mmoja wao