November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi wanawake Mkoa wa Arusha watakiwa kushirikiana kuifikia jamii na makundi mbalimbali

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Arusha

Mtandano wa Polisi wanawake mkoa wa Arusha umetakiwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi ili kuhakikisha kuwa wanaifikia jamii yote katika kutatua masuala mbalimbali hususani ya ukatili wa kijinsia.

Hayo yamesemwa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Justine Masejo wakati akizungumza na mtandao wa polisi wanawake mkoa wa Arusha katika tafrija fupi iliyoandaliwa na mtandao huo katika kilele cha siku ya wanawake duniani iliyofanyika katika ukumbi wa AICC Club jijini Arusha.

Pia amewapongeza askari waliofanya vizuri zaidi ambao walipewa vyeti pamoja na zawadi, ambapo aliwataka askari wengine kuchukua kama changamoto ambayo itakua ni chachu kwao kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kazi.

Kwa upande wake afisa mnadhimu namba moja wa Polisi Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtandao huo ACP Mary Kipesha amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mtaandao huo ni kuunganisha askari wote wa kike tanzania nzima pamoja na wanawake wengine katika taasisi mbalimbalil nje na ndani ya nchi ili kuboresha huduma kwa umma pamoja na kujenga imani kati ya Jamii na jeshi la Polisi.

Aliendelea kueleza malengo mengine ya mtandao huo ni kukabiliana na makosa ya ukatili wa kijinsia hasa wanawake na watoto, kujengeana uwezo kiutendaji, kushiriki katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kijamii, kuinuana kiuchumi, kielimu.

Tafrija hiyo ilihudhiriwa na maofisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wanawake mkoa wa Arusha