Na Mary Margwe,Times Majira Online,Babati
JESHI la Polisi mkoani Manyara linamshikilia mkazi mmoja wa Kijiji cha Ruksimanda kata na Tarafa ya Bashinet wilayani Babati mkoani Manyara, Regina Daniel ( 24 ) kwa tuhuma za kuua watoto wake watatu kwa sumu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, ACP Paul Kasabago amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema tukio hilo lilitokea Novemba 5, majira ya saa tatu za usiku mwaka huu huko katika kijiji cha Rukdimanda.
ACP Kasabago amesema, mama huyo aliwaua watoto wake watatu kwa kutumia sumu inayodhaniwa kuwa ni ya panya, ambapo alichokifanya alikuwa na ugomvi na mume wake kwa hiyo kwa ajili ya kumkomoa mume wake aliona ni bora akanunue maembe na sumu ya panya ambapo aliipaka kwenye maembe hayo na kuwalisha watoto wake.
Kamanda Kasabago amewataja watoto hao watatu waliouawa kuwa ni Emmanuel Augustino (7), Emiliana Augustino (4) na Elisha Augustino (1) wote watoto wa kuwazaa mwenyewe.
Aidha, amesema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Dareda Mission huko wilayani Babati, wakisubiria uchunguzi wa daktari na mara baada ya uchunguzi huo kukamilika miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
“Watoto hao walienda kufia katika kituo cha afya Bashinet walikokua wakipatiwa matibabu, miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Dareda Mission huko wilayani Babati, wakisubiria uchunguzi wa daktari, na mara baada ya uchunguzi huo kukamilika miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko,”amesema Kamanda huyo wa Polisi .
Aidha, ameongeza kuwa mama huyo ambaye aliua watoto wake anaendelea kushikiliwa katika kituo cha Polisi Babati wakiendelea na mahojiano naye na mara baada ya upepelezi kukamilika atafikishwa mahakamani kuhusiana na shitaka hilo.
“Lakini mama huyo ambaye aliua watoto wake tunaendelea kumshikilia katika kituo cha Polisi Babati, tukiendelea na mahojiano naye, na mara baada ya upepelezi kukamilika atafikishwa mahakamani kuhusiana na shitaka linalomkabili,”amesema Kasabago.
Kwa upande wa mmoja wa madiwani wateule wa viti maalum wilayani Babati, Magreth Kodi amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tukio la mama Regina Daniel kuua watoto wake watatu kwa kisa cha ugomvi wake na mumewe.
Magreth Kodi amesema,kitendo alichokifanya mama huyo ni kitendo cha kikatili uliopitiliza, kinachotakiwa kupigiwa vita mara moja ili akina mama wengine wasije wakapatwa na mihemko ya aina hiyo kwa watoto hao, chakushangaza kumekua na mashirika mengi yakipita kila wilaya kutoa elimu ya kukomesha vitendo hivyo, lakini bado anashangaa kuona wanawake ndio wanaoendelea na vitendo hivyo.
“Yaani mtu unagombana na mume wako unakuja kuwaadhibu watoto kwa kosa gani wao tena kama malaika wamekosea wapi hadi uamue kuwatoa uhai wao, watoto ni taifa letu la kesho sasa tunapowaua tunakua tumefanya nini sisi akina mama, mfano mimi leo ni diwani wa viti maalumu nimeingia kipindi cha pili nawatumikia wanawake na jamii mzima kiujumla ningeuawa ingekuaje leo, vivyo hivyo na hao watoto wetu watatu pengine baadaye tungepata madaktari au hata Rais, kwani huwezi kujua mipango ya Mungu,”amesema Diwani hiyo mteule.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi