December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi wamnasa mmiliki wa kiwanda cha silaha

Polisi wamnasa mmiliki
wa kiwanda cha silaha

Na Rotary Haule,TimesMajira Online,Pwani

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limemtia hatiani mtuhumiwa, Shabani Athumani (61) mkazi wa Chalinze Kwamakocho Kata ya Mandela kwa kosa la kumiliki kiwanda cha kutengenezea silaha mbalimbali za moto ikiwemo magobore.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 31,mwaka huu majira ya saa 1 jioni.

Nyigesa amesema kuwa, kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ilitokana na ushirikiano wa raia mwema na kwamba baada ya kupata taarifa hizo walifanya uchunguzi na kisha kubaini uwepo wa kiwanda hicho.

Amesema,katika uchunguzi huo Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa huyo akiwa na mtambo wa kufulia vyuma,chupa 5 ndogo zenye baruti ndani yake,Fataki 48 na risasi 42 za bunduki aina Gobole na Paketi 1 ya unga wa Kiberiti.

Wankyo ametaja vifaa vingine kuwa ni mitambo mitatu ya silaha aina ya gobore ambayo ipo tayari bado kuwekwa mtutu na kitako,mitambo ya kutobolea vifaa vya miti vinavyowekwa kwenye silaha aina gobore na kopo moja lenye unga wa tindikali ambalo unatumika kuunganisha vyuma vinavyofungwa kwenye silaha aina ya gobore.

“Mtuhumiwa tumemkamata akiwa anamiliki kiwanda cha kutengenezea silaha na vifaa vya silaha za kienyeji na uchunguzi bado unaendelea na baadae atafikishwa mahakamani,”amesema Wankyo.

Nyigesa amesema, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara moja kwa ajili ya kujibu tuhuma zake huku akiwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Aidha,katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa anamiliki bunduki tatu aina ya Shortgun na gobole moja,risasi 13 za Shortgun na maganda matatu ya risasi.

Kamanda Nyigesa amesema, mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 21, mwaka huu majira ya saa 6:30 usiku katika maeneo ya Pingo Wilaya ya Kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani.

Amesema kuwa,mbali na vifaa hivyo lakini vingine ni Cocking handle 2,gololi 60,misumeno miwili ya kukatia mbao na chuma, praizi moja,Bisibisi moja,kipande cha mtutu wa bunduki ,vipande vidogo vya chuma sita,vipande vya miti vyenye chuma ndani vinne na mitambo ya kutengenezea bunduki miwili.

Hata hivyo, Nyigesa amesema kuwa watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio hilo bado Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka na wakikamatwa watachukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani.