Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online,Songwe
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limeanika mbinu alizotumiwa mwanamke mchuuzi wa matunda, Severina Msongole (47) Mkazi wa kijiji cha Isangawana, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya kuiba mtoto wa miezi minne.
Kwa mujipo wa Polisi, mwanamke huyo maarufu kwa jina la Neema alifanikisha wizi wa mtoto huyo wa kiume, Evance Mwambogolo baada ya kumlewesha kwa soda inayodaiwa kuwekewa dawa mama yake, Maria Msyaliha (19) alipokuwa akiuza ndizi mnadani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 15, mwaka huu, saa nane mchana katika kijiji hicho cha Isangawana, Wilayani Chunya katika mkoa jirani wa Mbeya.
Amesema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 7, mwaka huu baada ya kununua ndizi mbivu za sh. 2,000 na kutengeneza urafiki uliosababisha kufanikisha tukio hilo.
“Mama wa mtoto wakati amepanga ndizi zake kwa ajili ya kusubiri wateja, ghafla alijitokeza mwanamke (Neema) aliyekuja kama mteja akanunua ndizi za sh. 2,000 na kutoa noti ya sh. 5,000,’ amesema na kuongeza;
“ Wakati muuzaji akihangaika kupata chenji ghafla mtuhumiwa alimuomba waongozane hadi nyumba ya kulala wageni alikofikia jirani na mnadani hapo ili akampatie fedha yake baada ya kukosa chenji na walipoingia chumbani alimpatia sh. 2,000 yake na kumkaribisha soda ”.
Kamanda Kyando ameongeza kuwa baada ya kupata kinywaji walitoka nje huku mtuhumiwa akimuomba mama wa mtoto huyo amsindikize mtuhumiwa kituo cha mabasi kwa kumsaidia kubeba mizigo aliyokuwa nayo na wakiwa njiani ghafla mzazi huyo alianza kujisikia kizunguzungu na kupoteza fahamu hali iliyompa mwanya mtuhumiwa huyo kuondoka na mtoto.
Hata hivyo Kamanda Kyando amesema baada ya mahohjiano alikiri kufanya tukio hilo ili kumridhisha mumewe wa sasa ambaye amekuwa akimsumbua mara kwa mara akitaka mtoto.
Amesema baada ya jitihada za kupata mtoto zilishindikana kutokana na kuwa na matatizo ya ujauzito kuharibika mara kadhaa.
Habari za uhakika kutoka kwa ndugu wa mtuhumiwa huyo, ambao hata hivyo waliomba kuhifadhiwa majina yao walisema mtuhumiwa ni mama wa watoto wanne na alitengana na mumewe kwa zaidi ya miaka 15.
“Mambo haya ni magumu sana, huyu mama (mtuhumiwa) alitengwa na familia yake kwa zaidi ya miaka 15 baada ya kuachana na mumewe, sasa naona hali ya upweke imesababisha ajitumbukize kwenye matatizo haya ya wizi wa mtoto,” amesema mmoja wa wanafamilia.
Amesema ugomvi wa kutengana na mumewe ulisababisha kuwa kabisa kuonana na watoto wake aliowazaa hivyo kwa zaidi ya miaka 15 aliishi bila kuwaona watoto wake.
***Kijiji Isangawana
Tukio la kukamatwa kwa Neema limezua taharuki kubwa kwa wakazi wa kijiji cha Isangawana Wilayani Chunya kwa kuwa waliamini kuwa mtoto huyo ni wake kwa kuwa muda alioishi hapo kabla ya kuondoka kwa miezi minne alionekana kuwa mjamzito.
“Neema aliondoka hapa Oktoba mwaka jana na kuaga kuwa anaenda kujitazamia hali yake kwao Mbozi…sasa hili la kuwa kaiba mtoto limetushangaza sana na hata alipofika juzi hapa tulimpongeza na kumshika mkono kwa Baraka za kupata mtoto,” amesema mmoja wa wauza matunda wenzake katika kijiji cha Isangawana.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi