April 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Mbeya kuimarisha ulinzi kuelekea sikukuu ya Pasaka

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

KUELEKEA Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kufanya misako na doria za magari, pikipiki, mbwa wa Polisi na miguu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo  amesema kuwa katika nyumba za ibada hususani kanisani, Polisi limejipanga kushirikiana na kamati za usalama zilizopo katika maeneo hayo.

Amesema kuwa katika makazi ya watu Jeshi la Polisi linaendelea na utaratibu wa kufanya doria kwa kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika maeneo hayo na katika kumbi za starehe linawataka wamiliki kuweka walinzi binafsi pamoja na kuzingatia taratibu zote za uendeshaji wa biashara zao kwa mujibu wa leseni na vibali.

Aidha,Kuzaga amesema kwa upande wa usalama barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawata madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia “usalama wao kwanza” na utii wa sheria za usalama barabarani bila shuruti ili kuepuka ajali. Ni marufuku kwa Dereva kutumia kilevi, Jeshi la Polisi limejipanga kutumia vipima ulevi kukabiliana na madereva watakaotumia vileo na kuendesha vyombo vya moto,

Amesema kuwa pia  Polisi imejipanga kudhibiti makosa hatari kama vile mwendo kasi na “wrong overtaking” hasa katika maeneo hatarishi kama vile mlima nyoka, mlima iwambi, Igawilo na barabara ya Mbeya – Chunya, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekamatwa kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Amesema polisi inaendelea  kutoa rai kwa wazazi katika msimu huu wa sikukuu kuzingatia ulinzi na usalama wa mtoto kwa kuhakikisha wanaimarisha uangalizi wa watoto ili kuwaepusha na vihatarishi na mazingira hatarishi. Hatutegemei kuona watoto wanazurura hovyo mitaani bila kuwa na uangalizi, kwenye sehemu za michezo ya Watoto tunatarajia kuwaona wazazi/walezi wakiwa na watoto wao ili kuangalia usalama

Sambamba na hayo, katika maeneo yenye fukwe kama vile Matema, Ngonga – Wilaya ya Kyela, Kisiba – Wilaya ya Rungwe na Ziwa Ngosi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaimarisha ulinzi pia linawataka wamiliki wa maeneo hayo kuweka walinzi na waangalizi kwani katika kipindi hiki kunatarajiwa kuwa na idadi kubwa ya watu wa rika tofauti watakaofika maeneo hayo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka

Aidha Kamanda Kuzaga amewataka wananchi mkoani Mbeya  kuzingatia usalama wao kwani ulinzi unaanza na mimi, wewe na sisi sote na kusema polisi ipo imara na linawahakikisha usalama wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya, wageni watakaofika mkoani Mbeya na hata wale watakaopita kuelekea mikoa jirani na nchi jirani kwa kutumia barabara ya TANZAM inayounganisha nchi ya Tanzania, Malawi, Zambia hadi Afrika ya Kusini.