January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi, LATRA wapiga faini mabasi yaliyozidisha nauli Arusha

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa kushirikaiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) wamefanya ukaguzi wa kushtukiza ili kubaini kama wananchi wanalipa nauli halali zilizotangazwa na Serikali mapema mwezi huu ambapo wamebaini baadhi ya wamiliki na mawakala wa mabasi kuwapandishia nauli wananchi huku mamlaka hiyo ikiwapiga faini kwa kosa la kuzidisha nauli hizo.

Akiongea katika ukaguzi wa nauli hizo mapema Jana katika kituo cha mabasi yaendayo Mikoani na nchi Jirani Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema wapo katika ukaguzi wa nauli kutokana na malalamiko ya wananchi kupitia simu na mitandaoo ya kijamii kuhusiana na kupanda kwa nauli.

Ameongeza kuwa kwa sasa ukataji tiketi ni kwa mfumo wa kielektroniki ambapo amesema kuna mifumo mipya inayorahisisha kuangalia bei elekezi ya serikali huku akiwaomba abiria kutumia mifumo hiyo ili kutokuumizwa na nauli kandamizi ambazo zinatozwa na baadhi ya mawakala na wamiliki wasio waaminifu.

Kwa upande wake Afisa mfawidhi wa mamlaka ya udhibiti usafiri Ardhini LATRA Mkoa wa Arusha Joseph Michael amesema kuwa wamefanya ukaguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuangalia utekelezaji wa masharti ya leseni za latra kwa mujibu wa usafirishaji huku akitoa onyo kwa wamiliki na mawakala kutokata tiketi bila kutumia mfumo wa kieletroniki.

Nae Joseph Peter ambaye ni abiria licha ya kupongeza Jeshi la Polisi na mamlaka hiyo amesema kuwa wao wamekuwa wakikata tiketi za mkono bila kufahamu madhara huku akiwaomba kutooa elimu zaidi ili kupunguza changamoto wanayoipata katika kukata tiketi ambazo zipo katika mfumo wa kimtandao.