Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Moshi
JESHI la Polisi nchini limesema limetengeneza mfumo madhubuti utaoongeza udhibiti wa uhalifu dhidi ya wanyamapori na maliasili katika viwanja vya ndege na mipaka ya nchi.
Lengo la mfumo huo ni kudhibiti mipaka na viwanja hivyo visitumike kinyemela kusafirishia bidhaa za maliasili na wanyamapori ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai nchini(DCI), Ramadhani Kingai, amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku Tano kwa wakufunzi wa Shule za polisi kuhusu biashara haramu ya usafirishwaji wa wanyamapori nje ya nchi.
Katika utekelezaji wa mfumo huo, jeshi la Polisi linakusudia kuanza rasmi kufundisha mtaala maalumu kuhusu athari za biashara hiyo katika vyuo vyote vya polisi nchini.
Kingai amesema Jeshi Hilo, litaendelea kuongeza udhibiti kwa kutumia mbinu za kisasa katika viwanja na mipaka ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kulinufaisha Taifa na siyo vinginevyo.
Amesema katika mafunzo kwenye vyuo hivyo polisi watajifunza, mbinu za Upelelezi na kuendesha mashauri kuhusu biashara hiyo ambayo inaathiri upatikanaji wa fedha za kigeni.
Kingai amesema mafunzo hayo ya wakufunzi 120, yanayotolewa kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Traffic International East Africa ni kuongeza mbinu mpya za Upelelezi, uendeshaji wa mashtaka wa kesi zinazohusu maliasili na wanyamapori.
Hata hivyo amesema kwa Sasa matukio ya ukamataji wa nyara za wanyamapori yamepungua kutokana na doria za mara kwa kushirikiana na askari wa hifadhi.
Katika hatua nyingine, DCI ametoa onyo kwa wote wanaopanga njama za kuendeleza ujangili kwani watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Awali mkurugenzi wa Traffic International East Africa, Julie Thomson amesema mafunzo hayo ni sehemu ya tathmini iliyofanyika Novemba mwaka 2021 kuhusu uelewa wa biashara haramu ya maliasili na wanyamapori.
Amesema tathmini hiyo ilifanyika katika vyuo vya polisi Zanzibar, Shule ya polisi Moshi na Dar es salaam na kubaini uhitaji mkubwa mafunzo ya uelewa na mbinu za kukabili biashara hiyo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best