January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Katavi yashiriki shughuli za kijamii

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

JESHI la polisi Mkoa wa katavi limeshiriki kufanya zoezi la usafi na uchangiaji damu katika hospitali ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya kusherekea maazimisho ya kilele cha miaka 60 ya Jeshi la hilo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi hilo leo Septemba 17, 2024,Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi David Mtasya amesema Jeshi la Polisi katika kusherekea maazimisho ya kilele cha miaka 60 ya jeshi hilo limeamua kufanya usafi na kutoa damu katika hospital ya wilaya ya Mpanda ili kuonesha kuwa jeshi hilo lipo karibu na jamii.

Mtasya amesema Jeshi la polisi limevutiwa kufanya zoezi hilo katika hospitali kwakua ni moja ya sehemu zinazo vuta hisia za watu wengi kuliko kwenda maeneo mengine lakini pia kuwasaidia watu wenye uhitaji wa damu ili kupunguza vifo vinavyo tokana na ukosefu wa damu kwa  makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Amesema hospitali ni sehemu inayo hitaji usafi wa hali ya juu katika kudhibiti mlipuko wa magonjwa ambayo yanababishwa na mrundikano wa uchafu. Kwa sababu hiyo jeshi la Polisi limeamua kushiriki kuongeza nguvu ya uwajibikaji katika kuhakikisha maeneo yote ni safi.

Katika hatua nyingine Mtasya ametoa wito kwa taasisi nyingine kushiriki kutoa damu,kufanya usafi na kuwasaidia wasio jiweza ili kuwa sehemu ya jamii yenye upendo na uajibikaji.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mpanda,Dkt.Paul Lugata amelishukuru Jeshi hilo kwa kuchangia damu  kwa sababu watu wenye uhitaji ni wengi  katika hospitali hiyo  akitaja ajali nyingi kuongezeka, Watoto wadogo kuishiwa damu na mama wajawazito  wanao jifungua kuishiwa damu makudi yote yanahitaji damu.

Vilevile amewashukuru askari walio jitolea kufanya usafi katika maeneo mbalimbali yanayo zunguka hospitali hiyo na kuwaomba waendelee kujitolea kushiriki kufanikisha mambo mbalimbali ya kuisaidia jamii.

Abdala Makwavi, Ni moja ya askari polisi walio changia damu amesema jukumu la askari polisi ni kulinda watu na mali zao lakini wameona vema jambo jema kuwa sehemu ya jamii katika kuhakikisha watu wenye uhitaji wa damu wanapata damu ili kuokoa  uhai wao.

Aidha Leo Septemba 17, 2024 ni kilele cha maazimisho ya miaka 60 ya Jeshi la polisi nchini ambapo maazimisho ya kitaifa yamefanyika Mkoa wa Kilimanjaro katika chuo cha mafunzo ya kijeshi Moshi.