Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Arusha
MKUU wa Wilaya ya Arusha, Kenani Kihongosi amemtia mbaroni Polisi (jina linahifadhiwa) akidaiwa kuiba umeme kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja.
Aidha, Polisi huyo amedaiwa kukutwa na misoko ya bangi, viroba vya pombe kali vilivyopigwa marufuku na Serikali ambavyo inadaiwa alikuwa akivijaza kwenye chupa za konyagi na kwenda kuuziwa wananchi.
Pia, ndani ya nyumba ya askari huyo inadaiwa kukutwa madumu mawili ya mafuta aina ya dizeli.
Akizungumza baada ya kumkamata askari huyo, DC Kihongosi amesema kuwa mtuhumiwa huyo alijiunganishia umeme kinyume na sheria kwa kuweka swichi chooni ambayo ilitumika kuiba umeme na kukwepa kulipa bili kwa mwaka mzima au zaidi ya hapo, kwani hawana uhakika.
Amesema baada kupekua nyumba anayoishi ya askari huyo pamoja na gari lake, walikuta pombe kali za viroba aina ya Konyagi.
DC Kihongosi amesema askari huyo amekua akivijaza katika chupa za Konyagi na kuwauzia wananchi katika baa. Alisema amekuwa akifanya hivyo katika mazingira ambayo si salama na hivyo hawawezi kujua ni watu wangapi wameathirika kwa unywaji pombe hiyo isiyokuwa salama.
Amesema amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) kumkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria akiwa na vielelezo hivyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, ACP Salum Hamduni ameahidi kutoa ufafanuzi wa tukio hilo hapo baadaye baada kukamilisha taratibu za kiofisi.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea