November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Poland yafurahishwa na ushirikiano baina yake na Tanzania

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Online

NCHI ya Poland imefurahishwa na ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania, ambapo imeahidi kuendeleza ushirikiano huo ili kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile inayohusu Sekta ya Mifugo nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Pawel Jablonsiki mara baada ya kufika na kukagua maabara ya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo iliyopo kwenye taasisi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Tengeru iliyopo jijini Arusha.

“Nimefurahishwa sana na kazi kubwa iliyofanyika hapa na nina imani miradi mingine inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Poland, itaendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa,” amesema Jablonsiki.

Balozi huyo amesema uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi yake ndio kitu kikubwa ambacho pande hizo mbili, zitaendelea kujivunia daima ambapo ameonesha kutambua na kuthamini mchango wa Tanganyika kwa nchi hiyo wakati wa vita kuu ya pili ya dunia.

“Ninaomba Katibu Mkuu unifikishie salamu kwa Waziri kwa sababu ninatambua kazi kubwa anayoifanya katika kukuza Sekta ya Mifugo nchini na sisi kama Poland, tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuboresha sekta hiyo hapa nchini,” amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Profesa Ole Gabriel ambaye alimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameishukuru nchi ya Poland kwa mchango wao katika kukuza sekta ya mifugo nchini, ambapo alimuomba Waziri huyo kuihakikishia Serikali ya Poland kuwa Wizara yake ipo tayari kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na nchi hiyo.

“Lakini jambo moja ambalo Waziri wangu amesema, nikuombe ni kwamba sasa maabara zimeshakarabatiwa zikiwa na vifaa vya kisasa, hivyo pale ambapo hali ya ugonjwa wa Corona itakapokuwa nzuri, tungependa kuwepo na mpango wa kubadilishana wanafunzi baina ya Tanzania na Poland,” amesema.

Amesema maabara hizo zilizoboreshwa kwa msaada wa nchi ya Poland, zitawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu masuala mbalimbali ya kitaalamu yanayohusu mifugo nchini ambapo aliahidi kuitunza miundombinu hiyo, ili iweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa LITA, Dkt. Pius Mwambene amesema nchi ya Poland imetoa ufadhili kwenye miradi sita ya taasisi hiyo, ambapo miongoni mwa miradi hiyo ni huo wa uboreshwaji wa maabara za mafunzo za taasisi hiyo Kampasi ya Tengeru.

“Mbali na maabara hizo, Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA), inatarajiwa kuwa na vituo vitatu vya umahiri ambapo Kituo cha Tengeru kitakuwa kikihusiana na masuala ya maziwa, Kituo cha Mabuki mkoani Mwanza kitajihusisha na masuala ya nyama na Kituo cha Morogoro, kitahusiana na masuala ya ngozi,” amesema.

LITA imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa mifugo nchini, lengo likiwa ni kuboresha sekta hiyo na kuifanya iendelee kutekelezwa kwa tija.