November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Paroko awataka vijana kuchangamkia elimu ya Ufundi

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

MKURUGENZI wa chuo cha ufundi cha St Anselim Vocational training Centre kilichopo Chala  ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Chala  wilayani Nkasi mkoani Rukwa Anselim Kashatila amesikitishwa na kitendo cha vijana waliokuwa wakisoma chuo hicho kuacha masomo na kwenda kuzurura mtaani licha ya masomo yao kutolewa bure chini ya wafadhili kutoka nchini Ujerumani.

Akizungumza jana kwenye mahafali ya kwanza ya chuo hicho amesema kuwa yeye katika urafiki na wenzake walioko Ujerumani walimwambia wamusaidie nini ndipo yeye alipoomba ajengewe chuo cha ufundi lakini pia hawakuchoka wakatoa na ufadhili bure wa masomo katika shule hiyo  lakini amesikitishwa baada ya kuona baadhi ya vijana waliofadhiliwa kukimbia masomo na kwenda kuzurura mitaani.

Alisema kuwa katika mpango huo wa ufadhili wa masomo waliandikisha Wanafunzi 57 lakini cha ajabu katika mwaka wa kwanza tu vijana 30 walikimbia masomo na kubaki 27 ambao mpaka jana walihitimu masomo yao huku wakiwa na ujuzi katika fani mbalimbali walizozisoma katika chuo hicho.

Hivyo amewataka wazazi wa Watoto wilayani Nkasi kuhakikisha vijana wao wanapata elimu ya ujuzi kwa kwenda katika vyuo mbalimbali vya ufundi kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuwakwamua Watoto kujikwamua kimaisha na kuwa licha ya wao kuhamasisha sana elimu ya dini lakini pia ni lazima kuendana na elimu ya dunia ili kuweza kukabiliana na na hari ya maisha kiuchumi.

‘’Elimu ya dini pekee haiwezi kuisaidia jamii bila ya kuwafudisha stadi za maisha na ni jukumu letu Wazazi kuhakikisha vijana wetu wanajifunza stadi za maisha kwa kuwapeleka shule na kuwapatia ujuzi utakaowasaidia kuendesha maisha yao’’alisema

Sambamba na hilo ameitaka jamii ya wilaya Nkasi na mkoa Rukwa kuhakikisha wanaitumia vyema fursa ya kuwapo kwa mvua nyingi katika mkoa kwa kutafuta elimu ya kilimo ili waweze kuitumia elimu hiyo katika kuzalisha mazao ya chakula na biashara na kuwa kila kitu ili kiweze kuleta tija ni kujifunza na kupata elimu yake stahiki kinyume cha hapo ni kufanya kazi chini wa kiwango na kutofikia malengo stahiki.

Awali mkuu wa chuo hicho Ramadhani Kimbondile alisema kuwa chuo hicho kimeanza rasmi mwaka 2022 na  kimekamilika kwa maana ya kuwa na walimu na vifaa vya kufundishia vya kutosha na kuwa wahitimu wanaotoka katika chuo hicho wanakua wameiva na kuweza kwenda kupambana vilivyo kwenye soko la ajira kulingana na kuivishwa vilivyo katika chuo hicho.

Alizitaja kozi zitolewazo katika chuo hicho kuwa ni Umeme wa majumbani,Ufundi bomba,kilimo mseto na uhazili na kuwa wahitimu walianza wakiwa 57 lakini waliohitimu ni 27 ambapo Wavulana ni 15 na Wasichana ni 12 katika kozi za Umeme wa majumbani ni 16 ambapo kati yao Wavulana ni 12 na Wasichana ni 4,Ufundi bomba ni 4 ambapo Wavulana ni 4 na Msichana 1 na Uhazili 7 na wote ni Wasichana.

Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali ambaye aliwakilishwa na katibu tawala wa wilaya Tonny Mkama aliwataka wahitimu hao wakirudi uraiani wakaunde vikundi kulingana na taaluma zao ili serikali iweze kuwasaidia kupitia utaratibu mpya wa mikopo ya Wajasiliami inayotolewa na serikali.

Alisema kuwa huko nyuma kulikua na fedha za mikopo kwa Vijana,Wanawake na makundi maalumu kutoka halmashauri lakini sasa kuna utaratibu mwingine mzuri unakuja juu ya mikopo hiyo na kuwa njia rahisi ni kuunda vikundi na kuwa wamoja na kuunganisha nguvu.

Mahafali hayo ya kwanza yalienda sambamba na kuonyesha ustadi wa Wahitimu katika fani mbalimbali walizozisoma kwa vitendo kiasi cha wazazi kuridhika na elimu itolewayo katika chuo hicho.

katibu tawala wa wilaya Nkasi Tonny Mkama akizungumza kwenye mahafari ya kwanza ya chuo cha ufundi cha Mt.Anselim Vocational Training Centre
Wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukadhiwa vyeti vyao