Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imepongeza Serikali kwa ujenzi wa nyumba 109 kwa waathirika wa maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba 2023 mkoani Manyara.
Kamati imetoa pongezi hizo Machi 17,2025 wakati wa ziara yao katika kitongoji cha Waret kilichopo wilayani Hanang Mkoani Manyara kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa nyumba 109 kwa waathirika pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi iliyojengwa katika kitongoji hicho.
Akizungumza mara Baada ya ukaguzi wa eneo hilo , Mwenyekiti wa kamati hiyo na Mbunge wa Vwawa,Japhet Hasunga, amesema wameridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyopo pamoja na thamani ya fedha iliyotumika unaakisi ubora wa kazi.
“Kwanza tunampongeza Daktari Samia Suluhu Hassan ambaye aliona hili pamoja na viongozi wengine wote waliosimamia mradi huu, tumeona fedha za umma zikitumika kwa ufanisi, na hii ni ishara nzuri ya usimamizi mzuri wa miradi ya kimaendeleo hivyo tuhakikishe tunailinda na kuendeleza kwa ubora unaohitajika ,”amesema Hasunga.
Katika taarifa yake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema, ujenzi wa nyumba hizo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika wa maporomoko hayo.
Pamoja na ujenzi wa nyumba, serikali imekamilisha ujenzi wa shule mpya ya msingi katika eneo hilo, yenye thamani ya zaidi ya shilingi ya milioni 490, ambayo mpaka sasa inahudumia zaidi ya wanafunzi 600, ikiwa na madarasa ya kisasa, ofisi za walimu pamoja na vyoo.
“Nyumba hizo zimejengwa katika eneo la Waret Kijiji cha Gidagamond, Kata ya Mogitu, Wilaya ya Hanang,Eneo zilipojengwa nyumba hizo lilikuwa linamilikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la Magereza na sasa eneo hilo linamilikiwa na Halmshauri ya Wilaya ya Hanang’”
“Aidha, ujenzi wa nyumba umefanyika katika viwanja 109 vya ukubwa wa mita za mraba 800 kwa kila kiwanja kati ya viwanja 226 katika Kitalu A. Kila n TC nyumba ina ukubwa wa mita za mraba 29 ikijumuisha vyumba vitatu vya kulala, sebule, baraza, jiko la nje, bafu na choo cha nje. Ujenzi ulisimamiwa na Timu ya Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Wizara ya Fedha; Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara; na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’”ameongeza Dkt.Yonaz.
Katika hatua nyingine,Dkt.Yonaz amebainisha kuwa,serikali ipo katika mchakato wa kufunga vifaa maalum vya ufuatiliaji wa mwenendo wa Mlima Hanang ili kutoa tahadhari za mapema endapo kutatokea hali isiyo ya kawaida kama maporomoko au mafuriko.
“Tumejifunza kutokana na janga hili, na sasa tunachukua hatua za kisayansi kuhakikisha tunazuia madhara makubwa siku zijazo,”amesema Dkt.Yonaz.
Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeongeza matumaini kwa wananchi wa Hanang, ambao sasa wanashuhudia juhudi za serikali katika kuhakikisha ustawi wao unaboreshwa ambapo Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi kwa ufanisi na uwazi.





More Stories
Rais Samia ataka watakao kwamisha huduma za ardhi kuchukuliwa hatua
Kapinga : Ni maono ya Dkt.Samia wananchi wote wapate umeme
SBL yawawezesha Wanawake,Vijana Kanda ya Ziwa