Na Mwandishi wetu,Timesmajira
KAMISHNA wa Kazi na Uchumi Kamisheni ya kazi Wiazara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Rashid Khamis Othman amesema kuwa Tanzania itajipatia heshima kubwa katika medani ya kimataifa kama ikiridhia mikataba sita ya Shirika la kazi Duniani (ILO).
Kamishna Othuman amebainisha hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha siku mbili kilichoratibiwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa kushirikiana na ILO cha uhamasishaji na ujengaji uwezo wa Mikataba sita ya Shirika la Kazi Duniani,alitaja mikataba hiyo ni pamoja mkataba namba C102,C121,C122,C155,CI87 na C189.
Amesema mikataba hiyo ambayo inalenga kuimarisha haki za msingi za wafanyakazi, usalama na afya sehemu za kazi, pamoja na kuhakikisha mazingira salama ya ajira, imekuwa sehemu ya mazungumzo ya muda mrefu kidogo baina ya ILO na Serikali ya Tanzania.

“Tanzania tayari tulisharidhia mikataba 37 ya ILO na kama tutakwenda kuridhia hii sita mengine basi tutatengeneza heshima nzuri na hasa ukizingatia kwamba mikataba hii kwa kiasi kikubwa tayari tunaitekeleza ikiwemo hata ile ya msingi inayohusika na usalama na afya kazini,” amesema
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Tucta, Rehema Ludanga amesema mikataba hiyo inalengo la kulinda utu, heshima za wafanyakazi, kuimarisha maslahi yao, kuhakikisha haki zao za msingi zinalindwa, na kutoa mwongozo madhubuti wa kushughulikia majeraha au ajali zinazotokea sehemu za kazi.

“Endapo tutafanikiwa jambo hili ninyi mliopo hapa mtakuwa mmefanikiwa kwa faida ya watanzania wote, sina shaka nah atua ambayo tumefikia maana tulipoanza ni parefu safari iliyobakia ni fupi, tuendelee kumuomba Mungu aweze kutusaidia ili jambo hili lifanikiwe,” amesema Ludanga
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Caroline Mugalla, Mratibu wa Mradi wa Kukuza Utambuzi na Kuboresha Mazingira ya Kazi kwa Wafanyakazi wa Nyumbani kama watoa huduma kutoka ILO ,Chiku Semfuko anesema kikao hicho kinaonyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha haki za wafanyakazi, ushindani wa biashara, na maendeleo ya ajira zenye staha nchini.

Ameeleza kuwa majadiliano yatakayofanyika kwa siku mbili yatatusaidia kuona hatua zilizofikiwa, changamoto zilizopo, na mikakati ya kuharakisha mchakato wa kuridhia na kutekeleza mikataba hiyo sita ya ILO.
“Tunawashukuru TUCTA kwa uratibu, na tunathamini ushiriki wa serikali, waajiri, na vyama vya wafanyakazi. Ushirikiano wa kijamii ndio msingi wa kazi za ILO, tutaendelea kutoa msaada wa kitaalamu wakati wote wa safari hii,” amesema Semfuko

Aidha Isaya Thomas kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) amesema wao wapo katika kuelimisha waajiri ili wapate uelewa juu ya mikataba hiyo inayolenga kuhakikisha haki za mfanyakazi na waajiri hazipotezwi badala yake zinalindwa.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani