December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Osha yawanoa wanahabari wa JOWUTA masuala ya usalama wa Afya mahali pa kazi

Na Penina Malundo, Timesmajira 

WAKALA  wa Usalama wa Afya Mahala pa Kazi (OSHA),wametoa mafunzo maalum ya usalama mahali pa kazi  kwa Waandishi wa habari wa  Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kwa  kuhakikisha elimu  hiyo inawafikia wafanyakazi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza  leo jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Hadija Mwenda wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari,amesema tathmini iliyofanywa na OSHA imegundua kuwa kuna uelewa mdogo kwa wadau juu ya kazi zinazofanywa na  Wakala hao.

Amesema hivyo ameona ni vema Osha kushirikiana na waamdishi wa habari katika katika kuhakikisha uelewa wa masuala ya usalama mahali pa kazi unakua na kuwafikia Jamii nzima.

“Tumejipanga kuhakikisha elimu ya masuala ya afya mahala pa kazi inatolewa kwa kundi hili tunaamini  kupitia waandishi wa habari  itawafikia wananchi wengini zaidi hasa  wafanyakazi ambao tunaamini wataelewa kwa undani zaidi juu ya usalama wa afya zao mahala pa kazi,”amesema.

Mwenda amesema kupitia mafunzo hayo  waandishi wa habari watapata fursa ya kupitishwa katika mada ya kujua sheria ya usalama mahala pa kazi,utoaji wa huduma ya kwanza kwa mtu anapopata tatizo lolote la Kiafya pamoja na kujua umuhimu wa wakala hao kwa mahala pa kazi.

“Tumetoa mafunzo haya ili waandishi wa habari nao wavitambue vihatarishi kwa sababu hakuna mazingira ya kazi ambayo hayana vihatarishi, kazi yetu sisi OSHA ni kuhakikisha vihatarishi hivyo havimuathiri mfanyakazi yoyote  ili aweze kufanya kazi kwa tija hata akistaafu basi astaafu akiwa na afya njema,” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma amesema wanatambua kuwa waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto nyingi katika maeneo yao ya kazi hivyo mafunzo hayo yatawafanya kupata uelewa na kuwa mabalozi wazuri.

“Tunatambua kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa waandishi wa habari na tunaimani kuwa ushirikiano huu tuliouanzisha na OSHA utadumu na tutaweza kuwafikia waandishi wa habari wengi zaidi nchini,” amesema

Naye Katibu Mkuu wa Chama hicho, Suleiman Msuya amesema chama hicho kinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na kwa sasa kina jumla ya wanachama 400 nchi nzima na kwamba maombi yao kwa OSHA ni kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanachama wao wengine waliopo mikoani.

Mafunzo hayo yamewashirikisha takribani waandishi wa habari wa Chama hicho 50 kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.