Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Dar
KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imeahidi kufunga mtambo mkubwa wa nshati safi ya kupikia katika Soko la Samaki la Kimataifa Feri jijini Dar es Salaam ambapo wajasiriamali wa soko hilo watakuwa na urahisi wa kuipata nishati hiyo na kwa gharama nafuu kwa ajili ya kukaanga samaki.
Hatua hiyo imekuja baada ya wajasiriamali wa soko hilo kutoa ombi kwa Kampuni ya Oryx Gas pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ilala ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge Muss Zungu baada ya kupokea ombi kutoka kwa wajasiriamali wa soko hilo walioomba kufungiwa mtungi mkubwa wa gesi wakiamini utawasaidia katika shughuli zao.
Ahadi ya kufungwa kwa mtungi mkubwa wa gesi imetolewa wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi 700 ya gesi ya Oryx kwa Baba na Mama Lishe wa soko la Samaki la Kimataifa Feri jijini Dar es Salaam leo Machi 22,2024.
Wakati anazungumza mbele ya wajasiriamali hao,Zungu amewahakikishia Mama Lishi na Baba lishe katika Soko la Samaki la Kimataifa Feri kuwa watafungiwa mtambo wa nishati safi ya kupikia ili kuwaepusha kutumia fedha nyingi kununua gesi kupitia mitungi midogo.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda mazingira kuwaweka wanawake katika nafasi nzuri ya kujiendeleza kiuchumi.
Zungu kabla ya kueleza hayo alipokea maombi ya wafanyabiashara hao kupitia kwa kiongozi Zone Namba 7 katika soko hilo, Said Mpinji aliyelalamika kuwa wanalazimika kutumia sh. 110,000 kila siku kujaza gesi ya kuendeshea shughuli za baba na mama lishe.
Hivyo Zungu amesema tayari amezungumza na kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, Benoit Araman na amekubali kufunga mifumo ya gesi ya kisasa kasha kusambaza huduma hiyo kwa wafanyabiashara hao kwa gharama nafuu.
“Mkombozi wetu ni Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ameanzisha kampeni ya nishati safi ya kupikia, kuhakikisha Watanzania wanaishi maisha mazuri.
“Oryx wamekubali kuweka mtungi mmoja mkubwa na mifumo ya usambazaji, kasha watasambaza huduma kwa mama na baba lishe waliopo hapa na kuwafungia mita halafu watakuwa wakilipia huduma kama wanavyofanya katika umeme,” amefafanua.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Benoit Araman amesema Oryx wamewafikia wajasiriamali hao kwa lengo la kutekeleza mkakati wa Rais Dk. Samia wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kulinda mazingira na afya za wananchi.
“Tangu Julai mwaka 2021, tulianza mkakati huu baada ya Rais Dk Samia kutangaza kuwa Serikali yake inataka kuona hadi mwaka 2030 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.”
Wakati huo huo Mwenykiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Abbasi Mtemvu aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, ameeleza kuwa ugawaji wa mitungi kwa baba na Mama Lishe hao ni utekelezaji wa Ilani huku akitumia nafasi hiyo kumpongeza Zungu kwa namna anavyowatetea wananchi wa jimbo lake.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kuendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi.Pia amewataka mama na baba lishe wa sokoni hapo kujiandaa kupokea mitaji kutoka serikali ili kunua biashara zao.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua