November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ongezeko la maji ziwa Tanganyika laathiri biashara ya samaki

Na Edward Kondela,TimesMajira online,Rukwa

SERIKALI imesema katika kipindi cha muda mfupi ujao inatafuta eneo kwa ajili ya kuweka mwalo na soko la muda la kuuzia samaki katika Kata ya Kasanga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, kufuatia mwalo na lililokuwa soko la kata hiyo kujaa maji baada ya kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiangalia moja ya majengo ya lililokuwa Soko la kuuzia samaki Kasanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo na kusikitishwa na namna ongezeko la kina cha maji ya Ziwa Tanganyika lilivyoharibu mradi huo ambao ulikuwa haujaanza kuleta mafaniko kwa wananchi kwa kuwa ulikuwa una viwango vya kimataifa kuanzia kuuza samaki na kuzihifadhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema hayo mwishoni mwa wiki baada ya kutembelea eneo hilo na kujionea uharibu mkubwa wa miundombinu ya soko na mwalo kufunikwa na maji na kubainisha kuwa wizara inatafuta eneo la muda huku ikitafakari pia mipango ya muda mrefu kujenga sehemu ambayo ni salama zaidi.

Majengo ya Ofisi ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) Kituo cha Kasanga, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa yakiwa yamejaa maji kutokana na kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kuongezeka na kusababisha athari katika eneo hilo ambapo mwalo umefunikwa na maji pamoja na Soko la kuuzia samaki Kasanga kujaa maji.

“Hii safari nimetumwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kuangalia hali ilivyo, kwa jinsi nilivyoiona hatuwezi kufanya chochote hapa nitamshauri wizara tutafute eneo lingine na tutenge fedha za kujenga mwalo mwingine tutafute eneo ambalo litafanyiwa tathmini, hata maji ya ziwa yakiongezeka kusitokee athari ya namna hii.” Amesema Dkt. Tamatamah.

Afisa Mfawidhi Msimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika Bw. Juma Makongoro (aliyevaa fulana ya mistari) akiongoza msafara wa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (hayupo pichani) kushuhudia namna ongezeko la kina cha maji katika Ziwa Tanganyika lilivyoathiri mwalo na Soko la kuuzia samaki Kasanga, viwanda viwili vya kuchakata samaki pamoja na hoteli moja ya kitalii na namna athari hiyo ilivyoharibu shughuli za wavuvi kujipatia kipato kupitia uwepo wa soko hilo.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/21 inayoishia Mwezi Juni mwaka huu, wizara ilikuwa imetenga Shilingi Milioni 78 kwa ajili ya ukarabati mdogo kwenye Soko la Kasanga, Shilingi Milioni 748 katika Soko la Kirando lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa na Shilingi Milioni 187 katika Soko la Muyobozi lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma, lakini ukarabati ulishindwa kufanyika katika masoko hayo kutokana na kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kuongezeka na kuanza kusababisha athari.

Akizungumzia athari iliyojitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya lililokuwa Soko la Kasanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, mara baada ya kutembelea eneo hilo katibu mkuu huyo amesema Soko la Kasanga ambalo lilianza kutumika Mwezi Machi Mwaka 2020 uwekezaji wake umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 1.3 ikiwa ni gharama ya miundombinu na vifaa mbalimbali vilivyowekwa na serikali na wadau ukiwemo Umoja wa Ulaya (EU) na kwamba limetumiwa kwa miezi isiyozidi miwili pekee ndipo maji yakaanza kujaa katika soko hilo na kushindwa kutumika.

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Uthibiti wa Ubora, Usalama na Masoko ya Samaki na Mazao yake kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga (aliyevaa kofia) akiangalia majengo ya lililokuwa Soko la kuuzia samaki Kasanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, baada ya eneo hilo kujaa maji kutokana na kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka na kuharibu miundombinu ya soko hilo, ambalo lilikuwa likiunganisha watu zaidi ya 1,000 kila siku kwenye shughuli mbalimbali.

“Pamoja na hayo mwalo ulikuwa na viwango vyote kwa maana ya maeneo ya kupokelea samaki, kuoshea samaki na kuwapima kabla ya kuuza, eneo la kuuzia samaki wabichi, eneo la kuzalisha barafu na vyumba vya kugandisha samaki, eneo la kukaushia samaki kwa moshi, pamoja na vichanja vya kuuzia samaki na dagaa.” Amefafanua Dkt. Tamatamah

Ameongeza kuwa eneo hilo lilikuwa linawasaidia sana wavuvi wakati wa mavuno mengi kwani walikuwa hawawezi kuuza samaki wote kwa wakati mmoja, hivyo walikuwa wakiwahifadhi na kuwauza kwa bei nzuri, lakini uwekezaji huo haujaweza kuleta manufaa kwa wananchi wa Kata ya Kasanga baada ya mwalo na soko kujaa maji kutokana na ongezeko la kina cha maji ya Ziwa Tanganyika.

Aidha, amesema kwa sasa hakuna sehemu maalum ya kushushia samaki hivyo wavuvi wanashushia maeneo mbalimbali ambayo hayana ubora, pia soko la kuuza samaki la Kasanga lilikuwa linaunganisha watu zaidi ya 1,000 kila siku kwenye shughuli mbalimbali.

Pia, kutokana na hali hiyo amebainisha uwepo wa biashara ya kuuza samaki kwa njia zisizo rasmi ikiwemo kupeleka nchi jirani ya Zambia baada ya kukosekana kwa soko la kuuza samaki katika Kata ya Kasanga.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Msimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda Kuu ya Tanganyika Bw. Juma Makongoro kufuatia kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka, amesema pia ofisi yao ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi, Kituo cha Kasanga imejaa maji na kutumia njia hiyo kuwatoa wasiwasi wananchi wa maeneo hayo kuwa ndani ya muda mfupi masoko yaliyoathiriwa na ongezeko la kina cha maji cha ziwa hilo yatarudi na wananchi kuendelea na shughuli zao.

Bw. Makongoro amewaasa wananchi ambao wanataka kuuza samaki nchi jirani ya Zambia kufuata utaratibu kwa kuwahusisha watu au makampuni yenye leseni za kusafirisha samaki kwenda nje ya nchi ili waweze kuuza samaki kwa njia halali badala ya kutorosha na kwenda kuuza kinyemela.

Naye Afisa Mifugo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Bw. Wilbroad Kansapa akimwakilisha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, amesema kujaa kwa maji katika Soko la Kasanga na viwanda viwili vya kuchakata samaki katika eneo hilo kuna athari kubwa kwa uchumi wa wananchi na halmashauri kwa ujumla.

Amefafanua kuwa halmashauri inategemea mapato kutoka sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na kutokana na athari ya maji kufunika mwalo na kujaa katika Soko la Kasanga bajeti iliyopangwa na halmashauri haitaweza kufikia malengo kwa kuwa wananchi walikuwa wanalipa tozo mbalimbali wanapouza samaki na sasa hakuna biashara ya samaki.

Nao baadhi ya wananchi walioathiriwa shughuli zao kutokana na kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kuongezeka na kufunika mwalo na kujaa katika Soko la Kasanga wamesema kwa kushirikiana na uongozi wa kata na kijiji wako tayari kutoa eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki ili wananchi waendelee na shughuli zao za kuuza samaki na kukuza viwanda vya kuchakata samaki vilivyopo katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Wameongeza kuwa kwa sasa ni vyema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikahakikisha wanasimamia uanzishwaji wa soko la muda pamoja na uwepo wa vifaa vya kutunzia samaki ili wasiharibike na pia kupewa ruhusa ya kuuza samaki wengine kwenda nchi jirani ya Zambia kwa kufuata taratibu zinazotakiwa.

Katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Rukwa, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akiwa katika Kata ya Kasanga ameshuhudia pia uharibifu wa hoteli ya kitalii ambayo sehemu kubwa imefunikwa kabisa na maji pamoja na kiwanda cha kuchakata samaki cha Alpha Tanganyika Flavour Limited kikiwa nacho kimejaa maji maeneo yote ya kiwanda hicho.