Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga katika kuendelea kuimarisha na kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali nchini.
Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,Hamza Johari wakati akizungumza na kwenye Mkutano maalumu na vyombo vya habari uliofanyika tarehe 19 Machi, 2025 katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kivukoni Jijini, Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo,Amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mafunzo maalumu kwa Mawakili wa Serikali nchini yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia Machi 24 hadi 28 , 2025 yakiwa na lengo la kuongeza umahiri na utendaji kazi wa Mawakili hao.
Amesema mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali ni sehemu ya kuimarisha utaratibu wa Mafunzo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Mawakili hao, pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika mapema mwezi Febuari, 2025 ambapo aliiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali.

“Mhe. Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaboresha na kuimarisha uwezo wa Mawakili wa Serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha,”amesema Johari
Johari ameeleza mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali yataendeshwa na wakufunzi wabobezi wa ndani na nje ya nchi, ambao watatoa mada mbalimbali zitakazo waimarisha mawakili hao katika Uandishi, Uingiwaji na Majadiliano ya Mikataba ya Kimataifa, Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara, na Uandishi wa Sheria.
“Kama mnavyofahamu Mhe. Rais anazidi kuifungua nchi, wigo wa uwekezaji unaizidi kupanuka hivyo sisi kama Wanasheria ni lazima tuhakikishe kwamba tunanyumbulika ili kuendana na kasi hiyo,”ameeleza Johari

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Mawakili wa Serikali kujifunza zaidi majukumu yao katika kuuvaa uzalendo na kulinda maslahi na usalama wa Taifa, ili waweze kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuzingatia Usalama wa nchi.
Johari amesema kuwa, Mafunzo hayo yatawasaidia Mawakili wa Serikali kuweza kujikumbusha Sheria zinazohusu foreign exchange, hati fungani na dhamana.
“Tunataka kuwa na Wanasheria na Mawakili ambao watakuwa na uelewa mzuri katika masoko ya fedha, masoko ya mitaji.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali nchi nzima kuhudhuria bila kukosa mafunzo hayo, huku akiziomba Wizara, Taasisi na Halmashauri kuwaruhusu na kuwawezesha Mawakili wa Serikali kushiriki katika mafunzo hayo kwani yatasaidia kuboresha utendaji kazi wao.
“Nitoe wito kwa Mawakili wa Serikali ambao hawajajisajili wafanye hivyo haraka sana ili waweze kuhudhuria mafunzo haya ambayo yatawasaida kuimarisha utendaji kazi wao,”Amesema Johari.
Sambamba na hilo, Johari ametumia mkutano huo wa Vyombo vya Habari kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya Uongozi wake pamoja na mafanikio makubwa ambayo Taifa imeweza kuyapata.
More Stories
NACTVET yawahakikishia wadau, usimamizi thabiti wa ubora wa elimu ya Ufundi na Amali
Wasira awataka Wenyeviti CCM kuiga mfano Mkoa wa Mbeya
MSD:Serikali inatekeleza mpango uchujaji wa damu