Josephine Majura na Sabato Kosuri, TimesMajira Online, Dar
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kushirikiana na Idara ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya Wizara ya Fedha na Mipango na pia Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuanzisha miradi mipya ambayo Serikali itaweka hisa zake.
Ametoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti na Wafanyakazi wa ofisi hiyo akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo.
Amesema faida ya kuongezeka kwa miradi mipya ni kuifanya Serikali kupata gawio kubwa zaidi ambapo fedha hizo zitaisaidia Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na mashirika yanayoendesha miradi hiyo kuongeza uwezo wake wa kiutendaji.
“Pamoja na agizo la kuhakikisha kunakuwa na miradi mipya, nataka mfanye ufuatiliaji wa matumizi ya kila Shirika au Taasisi ili kupata uhalisia wa utendaji kazi na matumizi yao ili kupunguza matumizi yasiyo kuwa ya lazima lengo likiwa ni kuongeza faida na kurudisha sehemu ya faida hiyo kama gawio kwa Serikali” amesisitiza Mhandisi Masauni.
Aidha, ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia Kitengo cha Utafiti kuendelea kufanya tafiti mbalimbali zenye kuibua changamoto za uendeshaji wa mashirika na kuzitafutia ufumbuzi ili yaweze kujiendesha kwa faida ili kuepuka hasara kwa Serikali.
Akizungumzia baadhi ya Mashirika kutokuwa na Bodi, Masauni, aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuanzisha Mfumo wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma, ambao unatumika kutambua hali za Bodi na kusaidia kupata wajumbe wa Bodi kwa wakati.
Ameeleza kuwa ni vema kuwa na Bodi hizo kwa kuwa husaidia kujenga uwajibikaji na utawala bora katika mashirika na taasisi za umma.
Masauni amesema kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina inatakiwa kushiriki katika kutoa maoni na ushauri kwenye majadiliano yanayohusiana na mikataba mbalimbali ya miradi mikubwa kwa kuwa Msajili wa Hazina ndiye mlezi wa mashirika hayo na mwenye dhamana ya kulinda maslahi ya umma katika miradi mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Bw. Athumani Mbuttuka, alisema katika miradi ambayo Serikali ina hisa na inaendeshwa kwa tija, imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kufanya tathimini na upelembaji, akitolea mfano katika kiwanda cha Sukari Kilombero kuwa uchambuzi wa upanuzi wa kiwanda hicho umeweza kusaidia kuokoa kiasi cha takribani Dola za Marekani 69.5 milioni ambazo ni zaidi ya Shilingi bilioni 161 kabla ya kutoa gharama za awali.
Pia uchambuzi na majadiliano na kampuni ya Inflight umewezesha kupatikana kwa gawio la Dola za Marekani takribani 687,516 sawa na shilingi bilioni 1.6 ambazo zitaanza kulipwa mwezi huu.
Mbuttuka aliahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Masauni ili kuongeza uwajibikaji katika ofisi hiyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Masauni yupo jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ambapo atatembelea ofisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
More Stories
Wafanyabiashara wakutana Dar,kujadili hali ya biashara
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo