November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira yaeleza mafanikio ya miaka 60 ya muungano Tanganyika na Zanzibar

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Makamu  wa Rais,Muungano na Mazingira imeeleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiwemo kasi ya utatuzi wa changamoto imeongezeka ambapo hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muu gano na Mazingira,Dk.Seleman Jafo ameyasema hayo jijini hapa leo,Machi 26,2024 wakati akizungumza na Waandiahi wa Habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana  kuelekea  Miaka 60 ya Muungano Aprili 26,2024.

Dkt.Jafo amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006 hadi sasa,Changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi.

“Changamoto nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho, Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi,”amesema.

Dkt.Jafo amefafanua kuwaSerikali  zote mbili ya Tanzania na Zanzibar  zimeweka Mwongozo rasmi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambavyo hushirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano.

“Vikao hivyo hufanyika katika ngazi tatu za Makatibu Wakuu, Mawaziri na kikao cha Kamati ya Pamoja ambacho Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesema

Ameeleza mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni mafanikio ya Kisiasa ambapo amesema Muungano umedumu kutokana na utashi wa dhati wa kisiasa waliokuwa nao Waasisi wa Muungano ambao uliwezesha vyama vya siasa vya TANU na ASP kuungana na baadaye kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) tarehe 5 Februari, 1977.

“Mafanikio haya yanatokana na utashi wa dhati wa kisiasa waliokuwa nao Waasisi wa Muungano na Viongozi walioendelea kuwepo madarakani,”amesema.

Kwa upande wa mafanikio ya Kijamii,Waziri Jafo amesema suala la ulinzi na usalama
Serikali zote mbili zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa masuala ya Muungano kwa ufanisi mkubwa ikijumuisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano.

“Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wetu mafanikio makubwa yamepatikana katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji, barabara, umeme, utoshelezi wa chakula pamoja na  ustawi wa jamii kwa ujumla.

Aidha amesema katika  huduma za elimu, Shule za Msingi zimeongezeka kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 20,562 mwaka 2024. Kati ya hizo, shule za Serikali ni 18,012 na za binafsi ni shule 2,550. Shule za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka shule 41 mwaka 1961 hadi shule 6,511 mwaka 2024. Kati ya hizo, shule 4,892 ni za Serikali na 1,619 ni za binafsi.

Pia huduma za afya zimeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi chote cha Muungano.

“Kutokana na uwekezaji huo, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote vimeongezeka kutoka vituo 1,343 mwaka 1960 hadi vituo 9,662 mwaka 2024. Kati ya vituo hivyo, Zahanati ni 8,043; Vituo vya Afya 1,176; Hospitali za Halmashauri 171; Hospitali zenye hadhi ya Wilaya 182; Hospitali za Rufaa za Mikoa 28; Hospitali zenye hadhi ya Mkoa 34; Hospitali za Rufaa za Kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya Kanda 11; Hospitali maalumu 6; Hospitali ya Taifa 1; na Hospitali Maalumu za Taifa 6.

“Mfanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano ni kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za maji, umeme na mtandao wa barabara. Upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 77 mwaka 2022. Aidha, upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2000 hadi 78 mwaka 2022. Vile vile, mtandao wa barabara za lami na zege mijini na vijijini umeongezeka kutoka KM 1,360 mwaka 1961 hadi KM 11,966 mwaka 2022,”amesema.

Pamoja na mafaniko hayo amesema mafanikio mengine ni masuala ya mazingira ambapo amesema Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti nchini ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Chimbuko la Ofisi ya Makamu wa Rais ni Muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano huo ulitokana na Hati ya Makubaliano ya Muungano (Hati ya Muungano) iliyosainiwa na Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Ikulu Zanzibar tarehe 22 Aprili, 1964.