Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuzindua kitabu cha Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa lengo la kuelimisha umma.
Kitabu hicho kitazinduliwa tarehe 26 Aprili, 2022 siku ya kilele cha Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya uzinduzi, Ofisi imepanga kuwa na mpango endelevu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu historia ya Muungano na masuala ya msingi kuhusu Muungano.
Inatarajiwa kuwa, Mpango wa elimu kwa umma utaongeza uelewa wa historia ya Muungano na masuala mengine muhimu kuhusu Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ameyasema hayo leo 20/04/2022 wakati wa Mkutano na waandishi wa habari akiambatana na Mawaziri wenzake wawili ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) – Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma
Dkt. Jafo alisema, Muungano unapotimiza miaka 58 ni jambo la kujivunia na hatuna budi kuendeleza mazuri yaliyopatikana kutokana na Muungano na kusisitiza kuwa maadhimisho ya Muungano kwa mwaka huu yataambatana na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelimisha umma kuhusu historia ya Muungano, tulipotoka, tulipo na tunapoelekea kupitia kongamono litakaloongozwa na wabobezi mahiri wa masuala ya Muungano ambao wataeleza kwa kina historia ya Muungano, Misingi ya Muungano na Mafanikio ya Muungano kutoka pande zote mbili za Muungano.
“Wananchi wa pande zote za Muungano wamezaliwa baada ya Muungano, hali inayoonesha wazi uwepo wa umuhimu wa utoaji wa elimu ya historia ya Muungano pamoja na masuala ya msingi yanayohusu Muungano” Jafo alisisitiza.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa kwa lengo lilelile la kuelimisha umma hasa vijana, yameandaliwa mashindano ya Insha kuhusu Muungano kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ambapo kutakuwa na washindi sita (3 kutoka Tanzania Bara na 3 kutoka Tanzania Zanzibar) ambao watapewa zawadi siku ya tarehe 26 Aprili, 2022. Insha hizo zinawapa fursa wanafunzi kuelezea historia ya Muungano; mafanikio na changamoto za Muungano; na nafasi ya vijana katika kulinda na kudumisha Muungano.
Kwa upande wake Waziri Simbachawene amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadhimisho na Sherehe Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameridhia kuwa Mikoa, Taasisi za Serikali na Vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama viadhimishe Maadhimisho hayo kwa kufanya shughuli za Kijamii katika maeneo yao ya karibu au Vikosi na Kambi zao kama vile kufanya usafi, kupanda Miti na kutoa huduma za afya. Kitendo hiki adhimu kitaleta hamasa kubwa, Umoja na mshikamano na kuuenzi Muungano wetu kwa heshima na taadhima kubwa.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Waziri Juma amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaenda sambamba na Maonesho ya Taasisi za Muungano yatakayoanza tarehe 22 Aprili 2022 mpaka tarehe 06 Mei 2022 pamoja na Kongamano litakaloenda sambamba na kumbukizi ya Miaka 50 ya Muuasisi wa Muungano Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti