Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imeipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utoaji wa elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka ambao ni fursa ya ajira.
Pongezi hizo zimetolewa jijini hapa leo Agosti 7,2024 na Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani maarufu kama Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni.
Ameeleza kuwa taka zinazozalishwa nchini kwa sasa zimekuwa ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.
“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu kuhusu fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira” amesema Jaji Mwaimu.
Aidha Jaji Mwaimu amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais na kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya uhifadhi wa mazingira kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa taka ni fursa iliyojificha na hivyo elimu kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani sio kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.
“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na namna zinavyotakiwa kutenganishwa” amesema Jaji Mwaimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais,Sarah Kibonde amesema Ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya habari.
Ameongeza kuwa katika kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa buluu, fursa zitokanazo na taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kupitia maonesho tuna nyaraka mbalimbali ambazo ni vitabu ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), vipeperushi, majarida ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau nk” amesema Kibonde.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki maonesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2024.
Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang