December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyumba mpya za maendeleo kuibadili Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Zanzibar

WIZARA ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi (WAMM), Zanzibar imetiliana Saini ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya ASER kutoka Uturuki kwa ajili ya Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Maendeleo Zanzibar.

Hafla hiyo ya utiaje Saini ya Makubaliano imefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Maisara, Unguja baina ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Mngereza Mzee Miraji na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Ertan Murat.
Dkt Mngereza alisema lengo la makubaliano hayo baina ya pande mbili hizo ni kuanzisha mahusiano ya kikazi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za maendeleo na za biashara kwa mkopo nafuu.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji (kushoto) na Mkurugenzi wa kampuni ya ASER, Bw. Ertan Murat (kati) wakisaini saini ya makubaliano ya Mradi wa ujenzi wa Nyumba za Maendeleo Zanzibar

Alifahamisha kwamba mradi huo unatarajiwa baada ya taratibu zote za makubaliano kukamilika kwa pande zote mbili wizara ya Ardhi na Kampuni ya ASER ikiwemo, mapendekezo ya Mradi wa nyumba na gharama zake, taratibu za kisheria, kulipa fidia, nk.

Alisema Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi inatarajia kuwa na Mradi mpya wa nyumba za Maendeleo Chumbuni Zanzibar ambapo mradi huo utajenga nyumba 1,000 lakini nyumba hizo zitajengwa kwa awamu hivyo awamu ya kwanza zitajengwa nyumba 500 na awamu ya pili nyumba 500 ili kukamilisha idadi hiyo.

Pia alisema Mradi huo utajenga nyumba za vila 50 eneo la Fumba huku maeneo ya Mombasa kwa Mchina Mradi utajenga nyumba 48 za gorofa(48 flats) na nyumba za Mji Mkongwe zitafanyiwa matengenezo/ukarabati.

Mapema Naibu Waziri Wizara hiyo, Juma Makungu Juma alisema Zanzibar kuna mahitaji makubwa ya nyumba hivyo Kampuni hiyo imeahidi kujenga nyumba hizo mara baada ya kukamilisha taratibu zote zinazohitajika.

Alisema ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kujengwa katika maeneo tofauti Unguja na Pemba ambapo utazingatia kipato cha kila mwananchi ili kuweza kuzimudu kwa lengo la kuboresha maakaazi bora.

Aidha alifahamisha lengo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ( SMZ) ni kuwapatia makaazi bora wananchi wake kutokana na uchache wa nyumba zilizopo hazikidhi mahitaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Shirika la Nyumba Zanzibar Mwanaisha Ali Saidi alisema Shirika la Nyumba Zanzibar limekabiliwa na changamoto ya kuwa na nyumba chache huku baadhi ya nyumba kua chakavu na zinahitaji ukarabati.

Alifafanua kwamba ujio wa kampuni hiyo ya Ertan umeleta faraja kwani baada ya kukamilika kwa Mradi huo Shirika la Nyumba Zanzibar litaweza kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya ASER, Ertan Murat ameishukuru Serikali ya Mapniduzi Zanzibar na Wizara ya Ardhi kwa kuichagua kampuni yake kufanyakazi nao, hivyo ameahidi atafanyakazi hiyo kwa uaminifu na kwa viwango vilivyohitaji katika ujenzi wa Nyumba za Maendeleo Zanzibar.